Maafisa wa Ukraine na Urusi wamekamilisha siku ya kwanza ya mazungumzo mapya yanayosimamiwa na Marekani huko Abu Dhabi, huku mapigano katika mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu vita vya pili vya dunia yakiendelea.
Mkutano huo wa siku mbili unaozileta pamoja pande tatu unakuja baada ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kusema Urusi ilikuwa imetumia mwanya wa usitishaji mapigano ulioungwa mkono na Marekani wiki iliyopita kuhifadhi silaha, ikiishambulia Ukraine kwa idadi kubwa ya makombora ya masafa marefu siku ya Jumanne.
Rustem Umerov, mkuu wa Baraza la Usalama na Ulinzi la Kitaifa la Ukraine, aliandika kwenye mtandao X kwamba “Kazi hiyo ilikuwa muhimu na yenye tija, ikilenga hatua madhubuti na suluhisho la vitendo,”
Afisa wa Marekani ambaye alizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, pia aliyaita mazungumzo hayo kuwa na tija na akasema yataendelea leo Alhamisi kuanzia asubuhi.
Akizungumza katika hotuba yake kwa njia ya video ya usiku, Zelenskiy alisema ni muhimu kwa mazungumzo hayo kuleta amani ya kweli na kutoipa Urusi fursa mpya ya kuendelea na vita. Zelensky aidha alisema washirika wa Ukraine walipaswa kutoa shinikizo zaidi kwa Urusi.
“Lazima ihisiwe sasa. Watu nchini Ukraine lazima wahisi kwamba hali inaelekea kwenye amani na mwisho wa vita, si kuelekea Urusi kwa kutumia kila kitu kwa faida yake na mashambulizi yanayoendelea,” Zelenskiy alisema.
Zelensky pia alisema Ukraine ilitarajia mazungumzo hayo yatasababisha ubadilishanaji mpya wa wafungwa hivi karibuni.
Muda mfupi baada ya mazungumzo kuanza, vikosi vya Urusi vilishambulia soko lililojaa watu mashariki mwa Ukraine kwa risasi na mabomu ya matawanyiko, na kuwaua watu wasiopungua saba na kuwajeruhi 15, kwa mujibu wa gavana wa eneo la Donetsk Vadym Filashkin.
Lavrov adai Zelenskiy hataki makubaliano ya amani
Wakati haya yakiarifiwa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov hapo jana alimshutumu rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwa kutotaka kusaini makubaliano ya amani kwani ingemaanisha mwisho wa taaluma yake ya kisiasa. Taarifa hiyo iliripotiwa na shirika la habari la serikali la Urusi, RIA.
Zelensky amesema anataka makubaliano, lakini hayuko tayari kukubaliana na masharti ya Urusi ambayo anasema ni sawa na kujisalimisha na hayuko tayari kuipa zawadi Urusi eneo ambalo jeshi lake halijashinda katika uwanja wa vita.
Zelensky ameiambia Televisheni ya France 2 jana Jumatano kwamba idadi ya wanajeshi wa Ukraine waliouawa katika uwanja wa vita kutokana na vita vya nchi hiyo na Urusi inakadiriwa kuwa 55,000.
“Nchini Ukraine, rasmi idadi ya wanajeshi waliouawa katika uwanja wa vita, iwe wataalamu au wale walioandikishwa jeshini, ni 55,000,” alisema Zelenskiy, katika mahojiano yaliyorekodiwa awali ambayo yalitangazwa Jumatano.
Zelenskiy aliongeza kuwa mbali na idadi hiyo ya waliouawa kuna idadi kubwa ya watu waliochukuliwa kuwa rasmi hawajulikani waliko.
Umoja wa Ulaya kuipa Ukraine mikopo mipya
Kwingineko nchi za Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuhusu masharti ya mipango mipya ya mikopo kwa Ukraine yenye thamani ya euro bilioni 90 kwa miaka ya 2026 na 2027 ili kusaidia mahitaji ya kijeshi na kiuchumi ya Ukraine.
Chini ya mipango hiyo, euro bilioni 60 zimetengwa kwa ajili ya matumizi yanayohusiana na ulinzi. Hata hivyo, Ukraine inaweza kutumia fedha hizo kununua vifaa vya kijeshi kutoka kwa makampuni yaliyo nje ya Ukraine na Eneo la Uchumi la Ulaya, kama vile Marekani, ikiwa bidhaa zinazohitajika hazipatikani.
Makubaliano hayo yanakuja baada ya majadiliano makali miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu jinsi ya kuunganisha fedha hizo mpya na vifungu vya kununua silaha zilizotengenezwa Ulaya.