Mazungumzo hayo yanafanyika wakati Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yakionya juu ya ongezeko la vifo vya raia na hatari ya kuendelea kwa vita vya muda mrefu vya kuchosha pande zote.

Wajumbe wa mazungumzo kutoka Moscow na Kyiv wamekutana tena leo katika mji wa Abu Dhabi, kwa siku ya pili mfululizo ya mazungumzo yanayolenga kumaliza vita vilivyoanza karibu miaka minne iliyopita. Mazungumzo hayo yanapatanishwa na Marekani, lakini hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu mafanikio yoyote.

Wakati mazungumzo yakiendelea, Urusi imeendelea kushambulia mtandao wa umeme wa Ukraine, katika kile wachambuzi wanakitaja kuwa ni mkakati wa kuwakosesha raia umeme na kudhoofisha morali ya taifa hilo. Mapigano yanaendelea kando ya uwanja wa mapambano wenye urefu wa takribani kilomita elfu moja katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Ukraine.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema kuwa wanajeshi wa Ukraine wapatao elfu 55 wameuawa tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake. Amesema pia kuna idadi kubwa ya raia na wanajeshi wanaochukuliwa kuwa hawajulikani walipo, hili likiwa ongezeko kubwa ikilinganishwa na takwimu alizotoa mapema mwaka huu.

Falme za Kiarabu Abu Dhabi 2026 | Mazungumzo ya amani ya pande tatu kati ya Urusi, Marekani na Ukraine ya mwezi Februari
Wajumbe wa Urusi, Marekani na Ukraine katika mazungumzo ya Abu DhabiPicha: UAE Ministry of Foreign Affairs/TASS/ZUMA/picture alliance

Mazungumzo ya leo pia yamehudhuriwa na mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff, pamoja na Jared Kushner, mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump, kulingana na maafisa wa Ukraine. Mazungumzo ya awali mwezi uliopitayaligusia suala nyeti la udhibiti wa mkoa wa Donbas, ambao Zelensky ameutaja kuwa kiini cha mzozo huo.

Msimamo wa Urusi

Kwa upande wa Urusi, mjumbe maalum wa rais Vladmir Putin, Kirill Dmitriev, amesema kuna maendeleo chanya, akiishutumu Ulaya na Uingereza kwa kile alichokitaja kuwa juhudi za kuchochea vita na kuvuruga mazungumzo ya amani.

“Kama mnavyofahamu, tunashirikiana kwa karibu na utawala wa Trump kurejesha mahusiano ya kiuchumi kati ya Urusi na Marekani. Tumekutana leo, na mazungumzo yanaendelea vizuri. Wapo kutoka Ulaya na Uingereza wanaojaribu kuvuruga mchakato huu, lakini kadiri wanavyojaribu, ndivyo inavyoonekana kuwa kuna maendeleo.”

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema bado ni mapema kutoa hitimisho lolote, akisisitiza kuwa mazungumzo bado yanaendelea na kwamba Rais Putin anapokea taarifa mara kwa mara kutoka kwa ujumbe wa Urusi.

Falme za Kiarabu Abu Dhabi 2026 | Mazungumzo ya amani ya pande tatu kati ya Urusi, Marekani na Ukraine yaliyofanyika mwezi Januari
Mazungumzo ya amani ya pande tatu kati ya Urusi, Marekani na Ukraine yaliyofanyika mwezi Januari Picha: UAE Government/REUTERS

Wakati huo huo, Urusi imesema iko tayari kwa ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo na Marekani, kuhusu mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia, lakini ikasisitiza kuwa mtambo huo lazima ubaki chini ya udhibiti wa Urusi. Hatma ya mtambo huo ni mojawapo ya masuala tata yanayojadiliwa katika juhudi za kusaka amani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu raia elfu 15 wameuawa na zaidi ya elfu 40 wamejeruhiwa tangu vita vilipoanza.Mashambulizi ya hivi karibuni ya droni yamesababisha majeruhi wapya mjini Kyiv, huku pande zote mbili zikiendelea kurushiana makombora na droni.

Huku mazungumzo yakiendelea, Ukraine imesisitiza kuwa inahitaji dhamana madhubuti za kiusalama kutoka Marekani na Ulaya ili kuzuia mashambulizi yoyote ya baadaye kutoka Urusi, ikionya kuwa amani yoyote lazima iwe ya kweli na siyo fursa ya kuendeleza vita kwa njia nyingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *