Mkataba wa kudhibiti silaha za nyuklia uliosainiwa kati ya Marekani na Urusi, mataifa mawili ambayo yanamiliki idadi kubwa mno ya vichwa vya nyuklia duniani, unatarajiwa kuisha Februari 5.

Mkataba wa Kupunguza Silaha za Kimkakati, au New START, ndio mkataba pekee wa kupunguza silaha za nyuklia unaozifunga Marekani na Urusi.

Unaweka ukomo wa idadi ya vichwa vya nyuklia vya kimkakati vilivyowekwa tayari na Marekani na Urusi kuwa 1,550 na unaweka kikomo cha idadi ya makombora ya balistiki yanayovuka mabara, makombora ya balistiki yanayorushwa kutoka katika nyambizi na ndege za kivita za kimkakati yaliyowekwa tayari hadi yasiyozidi 800.

Mwezi Septemba mwaka jana, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alipendekeza kabisa kuongeza muda wa mkataba huo kwa mwaka mwingine.

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba Rais Donald Trump mwezi Januari aliashiria kwamba anaweza kuruhusu mkataba huo uishe, akisema, “Ukiisha, umeisha.”

Endapo makubaliano mapya hayatafikiwa, mataifa hayo mawili, ambayo kwa pamoja yanamiliki karibu asilimia 90 ya akiba ya silaha za nyuklia duniani, hayatakuwa na ukomo wa uwezo wao wa nyuklia.

Trump pia amesisitiza haja ya mpangokazi mpya unaoijumuisha China, lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa na nchi zinazohusika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Februari 4 aliwaambia wanahabari kwamba makubaliano yoyote ya nyuklia ya siku za usoni na Urusi lazima yaijumuishe China.

Alisema kwamba kufanikisha udhibiti wa silaha wenye tija katika karne ya 21 “hakuwezekani” bila ushiriki wa China.

Wasiwasi unaongezeka kwamba hii inaweza kuchochea zaidi ushindani mpya wa silaha za nyuklia duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *