GEITA: WAKALA wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) wilaya ya Geita imefanikiwa kumkamata mtu mmoja (jina linahifadhiwa) kwa tuhuma za kuhusika na kilimo cha hekari 3.5 za bangi ndani ya hifadhi.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuendesha shughuli za kilimo hicho haramu kwenye hifadhi ya shamba la miti Geita lililopo katika eneo la kijiji na kata ya Lwamugasa wilayani Geita.
Ofisa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Geita–Lwamgasa, Aloyce Paschal ametoa taarifa hiyo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Geita ilipofika kuteketeza zao hilo haramu.
Amesema kukamatwa kwa mtu huyo ni matokeo ya msako endelevu unaofanywa na maofisa wa TFS kwa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti shughuli haramu ndani ya hifadhi.

“Kilimo hiki kilikuwa kazi kukitambua kwa sababu bangi hii inalimwa Katikati ya mahindi, akipanda hindi, mstari unaofuata anapanda bangi, ukiangalia shamba kwa mbali unaona mahindi”.
Amesema mtuhumiwa tayari amechukuliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi wa kina juu ya tuhuma zinazomkabili ili kung’amua mtandao mzima wa biashara hiyo haramu.
Amesisitiza kuwa operesheni za kudhibiti uharibifu wa hifadhi zitaendelea kufanyika mara kwa mara ili kulinda rasilimali za misitu na mazingira kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Lucy Beda ameongoza kamati ya ulinzia na usalama ya wilaya kutekekeza bangi hiyo huku akionya wakazi wa Geita kuacha kulima bangi kwa mkumbo.
Amesema kilimo hicho haramu kimebainika katika Shamba la Miti Geita–Lwamgasa ambalo lina jumla ya hekari 28,160 kutokana na watu wachache kutumia vibaya fursa ya uwepo wa hifadhi.

“Tuna jukumu la kuhifadhi misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, lakini tumebaini baadhi ya wananchi wanaingia ndani ya hifadhi na kufanya shughuli za kibinadamu”, amesema Lucy.