Dar es Salaam. Licha ya kusafiri na timu hadi Morocco, imefichuka kuwa kuna uwezekano mdogo kwa Yanga kumtumia Clement Mzize katika mechi yake dhidi ya FAR Rabat, Jumamosi wiki hii.
Mzize ni miongoni mwa wachezaji 24 wa Yanga waliopo Morocco lakini inaripotiwa kwamba hajawa tayari kwa asilimia miamoja kutumika katika mchezo huo muhimu.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga kimefichua kuwa Mzize amejumuishwa katika kikosi kilichoenda Morocco ili kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa jopo la madaktari wa Yanga.
“Madaktari hao pia wamesafiri na kikosi, hali inayompa nafasi Mzize kuendelea na programu maalum za kurejea taratibu kwenye ushindani bila hatari ya kukumbana tena na majeraha,” kimefichua chanzo hicho.
Kusafiri na timu kunamfanya Mzize aendelee kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari hao tofauti na iwapo mchezaji huyo angebaki Dar es Salaam.
Mzize amerejea kwenye kikosi baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki nane, akipambana na majeraha ya goti yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji. Kipindi hicho kilikuwa kigumu kwake na timu, kwani Yanga ilimkosa mmoja wa washambuliaji wake muhimu zaidi.
Jeraha hilo lilitokea Septemba 27, 2025, kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola. Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, lakini ushindi huo uliambatana na janga hilo.
Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize. Picha na Mtandao
Hali ya Mzize ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya kujiunga na majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambako alijitonesha tena jeraha hilo. Tukio hilo lilimlazimu kufanyiwa upasuaji na kuanza safari ya kurejea kwenye ubora wake wa awali.
Msimu uliopita, Mzize alifunga mabao 14 katika Ligi na matano michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akithibitisha thamani yake ndani na nje ya nchi.
Mbali na takwimu hizo, Mzize ameweka historia kubwa barani Afrika baada ya kutwaa tuzo ya Bao Bora la Mwaka Afrika katika tuzo za CAF zilizotolewa mwaka jana nchini Morocco.
Akizungumza wakati wa safari hiyo, kocha mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, aliweka wazi kuwa hawana mpango wa kumharakisha Mzize kurejea uwanjani.
Kocha huyo alieleza kuwa afya ya mchezaji ni kipaumbele kikubwa kuliko presha ya matokeo ya muda mfupi.
Katika mchezo dhidi ya AS FAR Rabat, Yanga itakuwa ikisaka ushindi au angalau sare ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Huu ni mchezo wa presha kwa pande zote mbili.