Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 4
Kwa kadiri inavyojulikana, ni nchi mbili pekee barani Afrika zinazomiliki ndege za kivita aina ya F-16, mojawapo ya ndege maarufu zaidi duniani kwa uwezo wake mkubwa wa mashambulizi ya angani.
Umiliki wa ndege hizi umetokana na mikataba ya ununuzi wa kijeshi kati ya nchi hizo na serikali ya Marekani, ambayo ndiyo mtengenezaji na msambazaji mkuu wa ndege hiyo.
Mojawapo ya nchi hizo ni Misri.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, mwaka 2015 serikali ya Marekani ilianza kusafirisha ndege nane za kivita aina ya F-16 kwenda Misri, hatua iliyokuja katika kipindi ambacho mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili yalikuwa yanaimarika.
Uboreshaji huo wa mahusiano ulifuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Mursi na kupanda kwa Abdel Fattah al-Sisi, ambaye uhusiano wake na Washington uliendelea kuimarika kwa utaratibu.
Taarifa kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Misri ilieleza kuwa vifaa hivyo vya kijeshi vingewasili ndani ya siku chache, huku ikithibitishwa kuwa sehemu ya mzigo huo ilihusisha ndege za F-16.
Nchi nyingine ya Afrika inayomiliki ndege za kivita za F-16 ni Morocco.
Mwaka 2007, serikali ya Morocco ilisaini mkataba na utawala wa Rais George W. Bush wa Marekani wa kununua ndege 24 za kivita aina ya F-16 kwa thamani ya dola bilioni 2.4 za Marekani.
Zaidi ya muongo mmoja baadaye, mwaka 2019, Morocco ilisaini mkataba mwingine na Marekani wa kununua ndege mpya za F-16 pamoja na kukarabati na kuboresha zile ilizonunua awali, katika makubaliano yaliyokadiriwa kugharimu takribani dola bilioni 4.
Kwa ujumla, Misri na Morocco ndizo nchi mbili barani Afrika zinazoaminika kuwa na idadi kubwa zaidi ya ndege za kivita aina ya F-16, jambo linalozipa nafasi ya kipekee katika ramani ya nguvu za anga barani humo.
Chanzo cha picha, Getty Images
Ndege ya kivita ya F-16 na majukumu yake ya kijeshi
Ndege ya kivita ya F-16 ilibuniwa ikiwa ndogo, nyepesi na yenye uwezo mkubwa wa mapambano ya angani.
Hata hivyo, kwa kadri teknolojia na mahitaji ya kijeshi yalivyobadilika, ndege hii imechukua majukumu mengi zaidi, ikiwemo kushambulia malengo ya ardhini, kupambana na meli, kufanya upelelezi, na kutumia makombora ya kupambana na ndege adui.
Kufikia mwaka 2015, F-16 ilikuwa ndege ya kijeshi iliyotumika zaidi duniani, huku zaidi ya ndege 2,000 zikiaminika kuwa bado ziko katika matumizi hai kote ulimwenguni.
Kimaumbo, F-16 ina urefu wa takribani mita 15 na upana wa mabawa wa mita 9.45. Inaendeshwa na injini ya turbofan yenye uwezo wa kuzalisha msukumo wa kilonewtoni 130, hali inayoiruhusu kufikia kasi inayozidi mara mbili ya kasi ya sauti.
Silaha zake ni pamoja na kanuni ya milimita 20 pamoja na makombora yanayobebwa chini ya mabawa yake, huku uzito wake wa jumla ukiwa karibu kilo 10,000.
Umaarufu wa F-16 miongoni mwa majeshi ya anga duniani unatokana si tu na muundo wake thabiti, bali pia na uzoefu na mafunzo yaliyopatikana kutokana na vita vya anga vya Vietnam, ambavyo vilibadilisha kwa kiasi kikubwa falsafa ya mapigano ya angani.
Katika karne ya 21, F-16 imechukua nafasi inayofanana zaidi na ndege ya kushambulia ardhini jukumu ambalo halikuwa miongoni mwa malengo ya awali ya wabunifu wake mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Hata hivyo, uwezo wake wa kuzoea mazingira na majukumu tofauti umeifanya ibaki kuwa chaguo muhimu kwa majeshi mengi ya anga.
“Kila penye mgogoro mkubwa duniani, kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa F-16 au mfumo wa kivita unaohusiana nayo,” anasema Robinson, mtaalamu wa masuala ya anga katika Jumuiya ya Kifalme ya Anga (Royal Aeronautical Society) nchini Uingereza.
Awali, F-16 iliitwa Fighting Falcon, lakini jina hilo halikupata umaarufu mkubwa.
Badala yake, ndege hiyo imeendelea kujulikana zaidi kwa jina la Viper.
Kwa mujibu wa Robinson, jina hilo lilitokana na muonekano wake na kipindi cha televisheni cha Battlestar Galactica kilichoonekana mwishoni mwa miaka ya 1970, ambapo ndege ya kubuniwa aina ya Colonial Viper ilionekana kufanana kwa kiasi kikubwa na F-16.
Hata leo, anaongeza, F-16 bado inaonekana kama ndege iliyotangulia wakati wake, kama chombo cha baadaye kilichobaki katika zama za sasa.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid