
Nchi wanachama wa Kundi la Marafiki Watetezi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa zimetoa taarifa ambayo imelaani hatua ya hivi karibuni ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jeshi Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC.
Taarifa hiyo iliyotolewa na kundi hilo jana Jumatano imesema: “Kundi la Marafiki Watetezi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa linalaani vikali hatua ya kusikitisha ya hivi karibuni ya Umoja wa Ulaya ya kuzusha tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vikosi vyake vya ulinzi vilivyoanzishwa kikatiba, yaani Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Nchi hizo wanachama wa Kundi la Marafiki Watetezi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa zimeeleza katika taarifa yao kwamba zinapinga vikali mbinu hizo za kisiasa na kusisitiza kwamba hatua hizo za kinyume cha sheria zilizochukuliwa na Umoja wa Ulaya Januari 30, 2026 dhidi ya sehemu moja ya vikosi vya ulinzi vya nchi huru ni ukiukaji wa wazi wa misingi ya kisiasa ya sheria za kimataifa, ikiwemo usawa wa mamlaka ya kujitawala ziliyonayo nchi zote na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi yoyote, na vilevile zinakinzana na maandiko na malengo yaliyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeelezwa kwamba, nchi zingine haziwezi kuchukua hatua kinyume cha sheria dhidi ya vikosi vya ulinzi vya nchi huru na vilivyoundwa kulingana na katiba ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuvibandika lebo zisizo na msingi za “ugaidi” au hatua za upande mmoja za kimabavu.
Nchi wanachama wa Kundi la Marafiki Watetezi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa zimesisitiza katika taarifa yao: “hatua kama za ukiukaji wa sheria zinaanzisha mfano hatari na kudhoofisha moja kwa moja juhudi za kweli za kupambana na ugaidi, huku hatimaye zikihudumia maslahi maovu ya makundi ya kigaidi na kupingana na ahadi zilizowekwa nchi mbalimbali za kupambana na uovu huo”.
Nchi wanachama wa Kundi la Marafiki Watetezi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa zimebainisha katika taarifa yao kwamba, zinatambua juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vikosi vyake vya ulinzi, hususan Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika kukabiliana na kuzuia ugaidi katika eneo, ikiwa ni pamoja na kupambana na kulishinda kundi la DAESH (ISIS), na wakati huo huo zinasisitizia mshikamano wao wa kudumu na wananchi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo ni moja wanachama mwanzilishi wa Kundi hilo.
Kundi la Marafiki Watetezi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa linajumuisha nchi 17, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Algeria, Cuba, Venezuela, Palestina, Nicaragua, Uganda, Belarus, Bolivia, Zimbabwe, na nchi zingine kadhaa…/