Dar es Salaam. Wakati juhudi za kukuza mapato ya ndani zikiendelea, utafiti mpya umebaini kuwa biashara na matumizi ya pombe haramu nchini yamefikia kiwango cha kutisha, yakihatarisha afya za wananchi na kusababisha Serikali kupoteza takribani Sh1.026 trilioni kila mwaka kutokana na kodi isiyokusanywa.

Utafiti huo unaonesha kuwa asilimia 61 ya pombe yote inayotumiwa Tanzania ni haramu, hali inayoifanya nchi kuwa miongoni mwa zilizo na kiwango kikubwa cha matumizi ya pombe zisizofuata sheria katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mbali na hasara za kiuchumi, watafiti wanaonya kuwa ongezeko la pombe haramu linaambatana na hatari kubwa kiafya, kutokana na uzalishaji usiozingatia viwango, matumizi ya kemikali hatarishi na ukosefu wa udhibiti wa ubora wa bidhaa hizo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, pombe haramu ni pamoja na zile ambazo hazijalipiwa ushuru stahiki, hazina vibali vya afya, au zinazozalishwa na kusambazwa kinyume cha sheria. Hali hii inahusisha pia vituo vya kuuza pombe visivyo na leseni, ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa pombe hizo kwa urahisi mitaani.

Utafiti unaonesha kuwa pombe haramu zimeenea katika makundi yote ikiwemo pombe kali, bia na divai huku pombe za kienyeji zisizo halali kama gongo, mbege, komoni, wanzuki, ulan­zi na dengerua zikichangia sehemu kubwa ya soko hilo.

Ingawa baadhi ya pombe hizo zina asili ya kitamaduni, wataalamu wamesema matumizi yake sasa yanaendeshwa zaidi na bei nafuu, ambapo kwa mfano gongo inaweza kuwa hadi asilimia 80 nafuu kuliko pombe kali halali, jambo linalovutia watumiaji wa kipato cha chini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa matokeo ya utafiti huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema ukubwa wa tatizo hilo unahitaji hatua za haraka na za pamoja.

“Upotevu wa zaidi ya shilingi trilioni moja kila mwaka unapunguza uwezo wa Serikali kugharamia huduma muhimu kama afya, elimu na miundombinu. Wakati huohuo, wananchi wanajiweka kwenye hatari kubwa kiafya,” amesema Londo.

Kwa mujibu wa utafiti, sehemu kubwa ya hasara ya mapato inatokana na gongo pekee, ambayo inakadiriwa kusababisha upotevu wa takribani Sh709 bilioni kwa mwaka, huku pombe bandia na zinazoingizwa kwa magendo nazo zikichangia kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Leodegar Tenga, amesema utafiti huo umefanyika ili kuziba pengo la takwimu sahihi kuhusu soko la pombe haramu, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likifanyika kwa siri nje ya mifumo rasmi.

“Bila takwimu sahihi ni vigumu kubuni sera na mikakati madhubuti. Sasa tuna picha halisi ya ukubwa wa tatizo na tunaweza kupanga hatua zinazotegemea ushahidi,” amesema Tenga.

Kwa upande wake, mshauri wa Euromonitor International, Benjamin Rideout, amesema walitumia mbinu mbalimbali ikiwemo ziara kwenye maeneo yanayouza pombe haramu, mahojiano na wadau na tafiti kwa walaji ili kupata taswira halisi ya soko.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Obinna Anyalebechi, amesema pombe haramu zinaua ushindani wa haki na kuhatarisha maisha ya walaji.

“Bidhaa hizi zinapunguza mapato ya Serikali, zinaharibu biashara zinazofuata sheria na kubwa zaidi zinahatarisha afya za wananchi. Ndiyo maana tunaunga mkono juhudi za kupambana nazo kwa kutumia ushahidi wa utafiti huu,” amesema.

Utafiti pia umebaini kuwa licha ya watumiaji wengi kufahamu hatari za kiafya za pombe haramu, bei nafuu, upatikanaji wa kirahisi na kukubalika kijamii vinaendelea kuchochea matumizi yake.

Kutokana na hali hiyo, watafiti wanapendekeza kuimarishwa kwa udhibiti wa malighafi kama ethanol, kuongeza ufuatiliaji mipakani na ndani ya nchi, kuimarisha elimu kwa umma kuhusu madhara ya pombe haramu, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa kama mifumo ya uhakiki wa stempu za kodi ili kudhibiti biashara hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *