Ripoti ya kampuni binafsi inayotoa huduma za mtandao wa intaneti, Proton inaonya kuwa nchi kadhaa zinaongeza hatua za kuzima mtandao wa intaneti ili kuzuia upinzani na kuchukua fursa hiyo kuimarisha mifumo ya udhibiti na uchujaji wa taarifa mtandaoni. 

Kampuni hiyo yenye makao yake Uswisi, inayojulikana kwa huduma za baruapepe na VPN zilizo na usimbaji fiche, imekuwa ikifuatilia kwa miaka kadhaa jinsi serikali za kiimla zinavyotumia mbinu za udhibiti kama sehemu ya mkakati wao wa kisiasa.

Meneja wa bidhaa wa Proton, Antonio Cesarano, amesema kuwa sasa wanaona ongezeko la serikali kama Iran na Myanmar ambazo baada ya kuzima intaneti kwa muda mrefu, zinarejea zikiwa na uwezo mkubwa zaidi wa kudhibiti upatikanaji wa taarifa mtandaoni.

VPN huwasaidia watumiaji kuunganishwa kwa usalama na kwa siri, na mara nyingi huwaruhusu kukwepa vizuizi vya serikali. Hata hivyo, kampuni ya Proton ina wasiwasi kuwa serikali zinatumia muda mrefu ambao intaneti imezimwa kuimarisha uwezo wa kupambana na matumizi ya VPN.

Aidha, kampuni ya Proton inaeleza kuwa katika baadhi ya nchi, uwezo wa udhibiti umeongezeka kwa kasi kubwa. Meneja wa VPN wa Proton, David Peterson, anasema hali hii inaweza kuashiria kuwepo kwa “udhibiti kama huduma”, ambapo teknolojia za udhibiti zinauzwa na nchi zenye uzoefu mkubwa, kama China, ambayo teknolojia yake ya “Great Firewall” imeripotiwa kutumiwa na Myanmar, Pakistan na baadhi ya nchi za Afrika.

Picha | VPN
Chapa ya VPN katika simu ya mkononi inayoonyesha usalama wa kuitumia VPN kuingia mtandaoni bila ya kubainisha eneo la mtumiaji.Picha: Rafael Henrique/ZUMAPRESS/picture alliance

Kuzima Intaneti kunazidi Kuwa kawaida

Ripoti hiyo inaonyesha pia kuwa kuzima intaneti kabisa kunazidi kuzoeleka, licha ya madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii. Proton imetaja matukio ya hivi karibuni nchini Iran, ambako intaneti ilizimwa kwa karibu wiki tatu wakati wa maandamano ya kitaifa; Uganda kabla ya uchaguzi; na Afghanistan mwaka uliopita. Iran pia ilizima intaneti kwa wiki moja katikati ya mvutano na Israel.

Proton inaonya kuwa hatua hizi ni hatari na zinagharimu raia kwa kiasi kikubwa, kwani shughuli za kiuchumi husimama. Kampuni hiyo inashirikiana na mashirika ya kiraia kufundisha watu jinsi ya kukabiliana na udhibiti huo, ingawa inakiri kuwa ni mchezo wa paka na panya.

Uganda | Mtumiaji mtandao Kampala
Mwanamume akitumia simu kufuatilia taarifa mbalimbali baada ya mtandao wa interneti kufunguliwa tena Uganda.Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP/Getty Images

Katika nchi kama Myanmar, ambako matumizi ya VPN ni kinyume cha sheria, serikali hutumia VPN bandia kama mitego ya kuwabaini wapinzani. Polisi pia huwakagua raia barabarani na kuchunguza simu zao. Kwa sababu hiyo, kampuni ya Proton imeanzisha teknolojia inayoficha programu ya VPN ionekane kama programu ya kawaida, kama kikokotoo au programu ya hali ya hewa.

Ripoti inaongeza kuwa matumizi ya VPN huongezeka sana kabla ya serikali kuchukua hatua za kukandamiza. Kabla ya kuzimwa kwa intaneti nchini Iran Januari 8, matumizi ya VPN ya Proton yaliongezeka kwa asilimia 1,000. Uganda ilishuhudia ongezeko la asilimia 890 kabla ya uchaguzi wake, na Venezuela iliona ongezeko la asilimia 770 mwanzoni mwa mwaka huu baada ya mabadiliko ya kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *