
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa, Mkataba wa New START, unaoweka mipaka ya silaha za nyuklia kwa madola mawili makubwa zaidi duniani yanayomiliki silaha hizo, yaani nchi hiyo na Marekani unamalizika rasmi leo tarehe 5 Februari, na kwamba hadi sasa Moscow haijapokea jibu lolote rasmi kutoka kwa Washington kuhusu kuoongezea muda mpya mkataba huo.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imeongeza kuwa, Russia itakuwa tayari kukabiliana na vikali na vitisho vinavyoweza kutokea, lakini itabaki kuwa wazi kwa mazungumzo baada ya kumalizika muda wa makubaliano hayo ya mwisho ya kimkakati ya udhibiti wa silaha iliyofikia na Marekani.
Septemba mwaka jana, Rais wa Russia Vladimir Putin alitoa hadharani pendekezo la urefushaji wa muda, akiahidi kuendelea kuheshimu mipaka ya mkataba huo wa silaha za nyuklia kwa mwaka mmoja mwingine baada ya kumalizika Februari 5, ikiwa tu Marekani nayo itakuwa na mtazamo huo.
“Mawazo yetu yameachwa bila kujibiwa kwa makusudi,” imeeleza taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Russia na kuongeza kwamba, Moscow sasa inadhani “kwamba pande husika katika New START hazifungwi tena na majukumu yoyote au matamko yanayolingana”.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeendelea kueleza kwamba, sambamba na hayo, Moscow ingali iko tayari kutafuta njia za kisiasa na kidiplomasia za “kuleta uthabiti kamili kwa hali ya kimkakati iliyopo kwa msingi wa mazungumzo ya kufikia kwenye suluhisho la usawa na lenye manufaa kwa pande zote mbili”.
Mkataba wa New START, ambao ulisainiwa mwaka 2010 na kurefushwa mwaka 2021, unaweka mipaka ya vichwa vya nyuklia vya makombora na mitambo ya makombora hayo ya kimkakati na kuweka mifumo ya usimamizi wa silaha hizo za Russia na Marekani.
Wakati huo huo, kumalizika muda wa mkataba wa New START kutayaacha madola hayo mawili yenye kubwa zaidi za nyuklia duniani bila uangalizi wowote za silaha zao za nyuklia…/