Tasnia ya muziki na burudani nchini Tanzania ilipata pigo kubwa Januari 3, 2026, baada ya kutangazwa kifo cha mtunzi, muimbaji na mpiga gitaa mahiri, Ally Star.
Msanii huyo alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu, baada ya kuugua kwa miezi kadhaa.
Mwanzo wa Ugonjwa
Kwa mujibu wa familia na watu wa karibu, Ally Star alianza kuumwa miezi kadhaa kabla ya kifo chake, akilalamikia maumivu ya mbavu na kifua, hali hiyo ilimlazimu kuanza kufuatilia matibabu katika hospitali mbalimbali, huku afya yake ikiendelea kudhoofika hatua kwa hatua.
Kulazwa Muhimbili
Baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya, Ally Star alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya kina, ambapo madaktari walifanya jitihada kubwa kumuokoa, lakini licha ya uangalizi maalum, hali yake haikuonyesha nafuu ya kuridhisha hadi alipofariki dunia Januari 3, 2026.
Taarifa ya kifo
Taarifa za kifo chake ziliposambaa, mshtuko na huzuni vilitanda kwa mashabiki, wasanii wenzake na wadau wa burudani mitandao ya kijamii ilifurika jumbe za maombolezo, wengi wakimtaja Ally Star kama msanii aliyetoa mchango mkubwa katika muziki na aliyekuwa na nidhamu na heshima kubwa ndani ya tasnia.
Safari ya kuzikwa Kilosa
Baada ya taratibu za hospitali kukamilika, mwili wa marehemu ulisafirishwa kutoka Dar es Salaam kuelekea Kilosa mkoani Morogoro kwa ajili ya mazishi, safari hiyo ilikumbwa na changamoto njiani, baada ya gari lililobeba mwili wa Ally Star kuharibika mara mbili hali iliyosababisha msafara kuchelewa kufika, jambo lililoifanya familia kuamua mazishi yafanyike leo asubuhi saa mbili.
Swala ya mwisho
Mwili wa Ally Star uliswaliwa nyumbani kwao Kilosa saa mbili asubuhi Februari 5, 2026, Swala hiyo iliongozwa na Shekhe wa Wilaya ya Kilosa, Nassoro Milambo, ndugu, jamaa, marafiki na waumini walijitokeza kwa wingi kumuombea marehemu, huku hali ya huzuni ikitawala eneo hilo.
Mazishi Makaburi ya Familia Mkwatani
Baada ya swala ya maiti, mwili wa Ally Star ulipelekwa kuzikwa katika makaburi ya familia yaliyopo Mkwatani, Wilaya ya Kilosa. Mazishi yalifanyika yakihudhuriwa na familia, viongozi wa dini na wananchi mbalimbali waliokuja kumpa heshima ya mwisho.
Kauli ya familia
Baada ya mazishi, mtoto wa marehemu, Hemed Ally, alizungumza kwa niaba ya familia, akieleza safari ya ugonjwa wa baba yake hadi kifo chake, pia aliwashukuru watu wote waliowafariji na kushiriki msiba huo, akibainisha kuwa Ally Star ameacha watoto sita.
Katika Burudani
Ally Star ataendelea kukumbukwa kama msanii aliyetoa mchango mkubwa katika muziki wa Tanzania, hasa katika uandishi, uimbaji na upigaji wa gitaa akipata umaarufu zaidi akiwa na bendi ya TOT. Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya burudani, lakini kazi na mchango wake vitaendelea kuishi mioyoni mwa wengi.