ARUSHA: TANZANIA imeendelea kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwenye sekta za afya, kilimo, uhifadhi wa chakula na maandalizi ya nishati mbadala, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi na kuandaa mazingira ya kuanzisha nishati ya nyuklia kwa maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Profesa Najat Kassim Mohamed, mara baada ya kupokea ujumbe kutoka Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA).

Ujumbe huo umeongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi kwa Afrika wa IAEA, Gashaw Gebeyehu Wolde, akifuatana na Ofisa wa Usimamizi wa Programu wa shirika hilo, Kashlan Azza ambapo ziara hiyo inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na IAEA katika sekta za viwanda, afya, elimu, kilimo na chakula.

Amesema kwa sasa TAEC inatekeleza miradi minne mikubwa ya kimkakati kwa kushirikiana na Serikali, wadau wa ndani na wa kimataifa ambapo mradi wa kwanza kuwa ni uboreshaji wa mbegu na kuongeza tija ya kilimo kwa kutumia teknolojia ya nyuklia, unaotekelezwa katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Afrika (NM-AIST), kwa lengo la kuzalisha mazao bora na yenye ustahimilivu kwa wakulima wa Tanzania.

Mradi wa pili ni ujenzi wa maabara ya kisasa ya mifugo Zanzibar, unaotekelezwa kwa ushirikiano na maabara za kimataifa kutoka Vietnam, kwa lengo la kuchunguza magonjwa ya wanyama, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza sekta ya mifugo kwa kutumia sayansi ya kisasa.

Alisema mradi wa tatu ni ujenzi wa kituo cha matumizi mbalimbali ya mionzi (Multipurpose Irradiator Facility) jijini Dar es Salaam, kitakachotumika kuhifadhi chakula, kuua vimelea na kuongeza muda wa matumizi ya mazao bila kuhatarisha afya za walaji ambapo  upo katika hatua nzuri za ujenzi.

Kwa upande wa mradi wa nne, Profesa Najat alisema unalenga kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani nchini, ambapo idadi ya vituo itoongezeka kutoka viwili hadi sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *