Hasira na maswali mengi yanaendelea kuibuka nchini Senegal, kufuatia tuhuma nzito dhidi ya kampuni ya Kichina ya Softcare, inayotengeneza taulo za kike na nepi za watoto.
Mwisho wa mwaka jana, Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa nchini Senegal, ARP, ilidai kuwa Softcare ilipatikana na takribani kilo 1,300 za malighafi zilizokwisha muda wake wa kutumika, na bidhaa nyengine zisizofaa ikiwemo plastiki ambazo zinadaiwa kutumika katika utengenezaji wa bidhaa zao.
Baada ya ukaguzi huo ARP iliagiza bidhaa za Softcare ziondolewe sokoni hadi taratibu za uzalishaji zitakapohakikiwa upya.
Lakini siku chache baadaye, uongozi wa mamlaka hiyo ulitoa kauli mpya ukisema nyaraka za Softcare zinaonyesha kuwa malighafi hizo hazikuwahi kutumika.
Hata hivyo, wakaguzi waliokuwa kwenye kiwanda walishikilia msimamo wa ripoti yao, na hapo ndipo mitandao ya kijamii ikaanza kusheheni malalamiko ya watumiaji waliodai kupata muwasho baada ya kutumia bidhaa hizo.
Madaktari na wataalamu wa afya nchini humo wameonya kuwa bidhaa za usafi zinapozalishwa kwa malighafi zisizofaa zinaweza kusababisha muwasho, mzio, au hata maambukizi.
Baadhi ya wanawake wamejitokeza hadharani kudai kwamba walipata madhara baada ya kutumia taulo za kike za Softcare.
Softcare yenyewe inasema malighafi zinazolalamikiwa hazijawahi kutumika na kwa sasa zimehifadhiwa kwenye ghala linalosubiri kuteketezwa.
Serikali ipo kimya
Sakata hili lilichochea maandamano na Mbunge wa upinzani Guy Marius Sagna ameituhumu serikali kwa kukaa kimya kwa muda mrefu, huku wanaharakati wakisema mamlaka “zinachelewesha” kutoa majibu ya kina. Bunge la Senegal sasa limeanzisha uchunguzi maalum kuhusu hatua za kuondoa na baadaye kurejesha bidhaa hizo sokoni.
Aidha, sakata hili limezidi kutanuka baada ya kiongozi wa ukaguzi, Moussa Diallo, kudai kuwa alikataa rushwa kutoka kwa mawakala wa Softcare madai ambayo kampuni ya Softcare imekanusha ikisema ni ya uongo na yanayolenga kuchafua taswira yake.
Madai haya sio tu nchini Senegal, nchini Cameroon, watumiaji walishawahi kulalamika kuhusu muwasho na hisia za kuchoma baada ya kutumia bidhaa za Softcare, ingawa kampuni mama ilidai bidhaa feki ndizo zilikuwa zinasambaa sokoni.
Wataalamu wanasema wasiwasi kuhusu ubora wa pedi za kike barani Afrika bado ni mkubwa. Utafiti uliofanywa Kenya mwaka 2025 ulibaini tofauti kubwa za ubora kati ya chapa mbalimbali, na mara nyingi viwango vya usafi havikuzingatiwa ipasavyo.
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwenye uchunguzi unaoendelea nchini Senegal, huku watumiaji wakisubiri majibu ya uhakika kuhusu usalama wa bidhaa wanazotegemea kila siku.
//AFP
