Arusha. Waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kati wameanza kupatiwa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi wa kuandika habari za kiuchunguzi zinazohusu masuala ya mazingira.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanayodhaminiwa na shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) yametolewa leo Februari 5, 2026 na Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu Tanzania(THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za asili(MAIPAC) Mkoani Arusha.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa programu na uendeshaji wa THRDC, Halima Sonda, amesema wanahabari wanajukumu kubwa la kuhakikisha dunia na wananchi wanakuwa salama katika jamii inayowazunguka.

Aidha, amesema dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira, hivyo akawataka kutumia taaluma yao kuokoa dunia na wananchi kwa ujumla.

Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo yanayohusu habari za kiuchunguzi za mazingira.

“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuandika vyema habari za mazingira, uchafuzi mazingira, ukataji miti na uchimbaji holela wa madini”amesema

Naye, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma amesema ni muhimu wanahabari kujikita kuandika vyema habari za mazingira kwani zina mahusiano makubwa na haki za binadamu kutokana na athari ambazo zinaweza kujitokeza za kimazingira.

Mussa amesema,  THRDC na MAIPAC inakusudia kutoa mafunzo kwa wanahabari 140 nchi nzima kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi, ukataji miti, uchafuzi wa mazingira, kudhibiti taka ngumu na masuala ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori na sheria mbalimbali za mazingira na ardhi.

“Kuna habari nyingi zinahitaji uchunguzi, ikiwepo umuhimu matumizi ya nishati safi na kuachana na kukata miti, uvamizi wa watu maeneo ya jamii za asili kama Wahadzabe na kufungua mashamba,uchimbaji holela wa migodi na matumizi ya kemikali zenye madhara, kuzagaa kwa taka ngumu,”amesema Mussa

Kwa upande wake, Wakili Paulo Kisabo amesema, masuala ya mazingira yana uhusiano mkubwa na haki za binaadamu, hivyo ni vyema Kila mwandishi aliyepata mafunzo hayo akatumia vyema kalamu yake katika kutoa elimu kwa jamii ili iweze kujikinga na athari za kimazingira.

Aidha, amewasisitiza waandishi wa habari kuhusu sheria mbali mbali za kimataifa na ndani ya nchi kuhusiana na masuala ya haki za binaadamu, mazingira na uhuru wa kujieleza.

“Wanahabari fanyeni kazi kwa kuzingatia sheria. Mnalindwa na sheria nyingi za ndani ya nchi, hivyo mkizitumia vizuri kalamu zenu mtalisaidia kwa kiasi kikubwa taifa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *