Rais wa Marekani, Donald Trump, na mwenzake wa China, Xi Jinping, walizungumza kwa simu Februari 4. Trump alisema wana uhusiano “mzuri sana”, na kwamba walijadili masuala mbalimbali ikiwemo juu ya Taiwan, Ukraine, na hali nchini Iran.
Trump alitangaza mazungumzo hayo ya “muda mrefu na ya kina” kwenye mtandao wa kijamii. Amesema, pia walizungumzia ununuzi wa China wa mafuta, gesi, na bidhaa za ziada za kilimo za Marekani. Alielezea mazungumzo hayo kuwa “yote mazuri sana.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitoa taarifa kuhusu mazungumzo hayo. Ilisema Xi alisisitiza kwamba suala la Taiwan ndilo “muhimu zaidi” katika uhusiano wao. Alionya kwamba Marekani lazima ishughulikie kwa “busara” suala la kuiuzia Taiwan silaha.”
Utawala wa Trump mwezi Desemba mwaka jana uliamua kuidhinisha mpango wa jumla wa kuuza silaha kwa Taiwan, ambao ulikuwa na thamani ya dola zaidi ya bilioni 11. China ilipinga vikali hatua hiyo.
Yalikuwa ni mazungumzo yao ya simu ya kwanza tangu Novemba mwaka jana. Trump anatarajiwa kuzuru China kwa mkutano wa viongozi wakuu mwezi Aprili.