Zanzibar. Hatimaye leo Februari 5,2026 pazia la tamasha la Sauti za Busara, linalokutanisha wasanii zaidi 400 dunia linafunguliwa.
Tamasha hilo ambalo linafanyika Unguja, Zanzibar, mwaka huu linaenda na kaulimbiu isemayo ‘Let Them Shine’ ‘Waache Wang’are’. Huku likisisitiza wasanii kutumia vipaji vyao kuwa sauti ya haki kwa watoto.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania Elke Wisch, amesema UNICEF inawaomba wasanii wanaoshiriki tamasha hilo kutumia majukwaa yao kukuza haki za watoto, kupinga mila na mitazamo potofu inayodhuru, na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii.
Amesema muziki na maeneo mengine ya ubunifu yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwaunganisha watu na kuchochea mabadiliko chanya. Wasanii wana uwezo wa kipekee kufikia hadhira pana, hususan katika matamasha kama Sauti za Busara, ambako watu hutoka maeneo mbalimbali kushiriki uzoefu wa pamoja.
“Kaulimbiu ya tamasha inatukumbusha kuwa kila mtoto huzaliwa na uwezo, kipaji na mwanga ndani yake. Hata hivyo, ili mwanga huo uangaze kikamilifu, watoto wanapaswa kukua wakiwa salama, wakilindwa na kuungwa mkono sio tu na familia, jamii zao, bali na sisi sote tukishirikiana,”amesema Elke
Naye Nabiha Kassim, Mwakilishi wa Vijana wa UNICEF amesema mtoto hawezi kung’aa ikiwa anakumbana na ukatili katika mazingira yoyote, ikiwa anaishi kwa hofu, unyanyapaliwa au maumivu ya kimya na changamoto za afya ya akili
Hatahivyo kwa upande wake Journey Ramadhani ambaye ni Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara ameendelea kuukumbusha umma kuwa tamasha hilo toleo la 23 linafanyikia viwanja vya Mnazi Moja.
“Baada ya zaidi ya miongo miwili katika eneo moja, tamasha limekua kwa ukubwa na mahitaji, na mwitikio wa toleo la mwaka huu umeonyesha wazi kuwa tunahitaji eneo kubwa zaidi na lenye kubadilika. Wakati huohuo, Ngome Kongwe iko kwenye ukarabati, hivyo huu ni wakati muafaka wa kuchunguza fursa mpya.
“Kile ambacho hakijabadilika ni dhamira yetu ya ubora. Hadhira iendelee kutarajia tamasha kubwa zaidi mwaka huu, huku tukidumisha viwango na maadili yale yale yaliyoitambulisha Sauti za Busara kwa zaidi ya miaka ishirini.”
Kuhusu wasanii, Journey amesema orodha ya wasanii wa mwaka 2026 inaakisi kile ambacho Sauti za Busara inasimamia. Maonesho bora , utofauti wa sauti, na wasanii waliokita mizizi katika urithi wao.
“Kuanzia msanii mkuu wa tamasha Salif Keita kutoka Mali, hadi sauti zinazoongoza na zinazoibukia kutoka Tanzania, Afrika Kusini, Rwanda, Kenya, Uganda, Algeria, Nigeria na kwingineko, programu hii inawakutanisha vizazi na mitindo mbalimbali ya muziki.
“Zaidi ya majukwaa ya maonesho, tamasha linaendelea kuwekeza kwa wasanii kupitia majukwaa ya mitandao kama Movers and Shakers, yakitoa nafasi ya ushirikiano, kujifunza, na ukuaji wa muda mrefu ndani ya tasnia ya muziki barani Afrika.” amesema