Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mazungumzo kati ya Iran na Marekani yamepangwa kufanyika Oman Februari 6.
Taarifa hiyo mpya inakuja huku utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, ukiongeza shinikizo kwa Iran kufanya mazungumzo juu ya mpango wake wa nyuklia.
Meli ya kivita ya USS Abraham Lincoln inayoendeshwa kwa nguvu za nyuklia imepelekwa katika eneo la Bahari ya Arabia karibu na Iran.
Februari 4, Araghchi alisema kwenye mtandao wa X kwamba mazungumzo ya nyuklia kati ya nchi hizo mbili yatafanyika Februari 6 asubuhi katika mji mkuu wa Oman, Muscat.
Kabla ya hapo, Shirika la Habari la Tasnim, ambalo lina uhusiano na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, liliripoti kwamba mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja yatajikita tu katika mpango wa nyuklia wa Iran na kuondoa vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Ilisema Iran itawakilishwa na Araghchi, huku mjumbe maalum Steve Witkoff akiiwakilisha Marekani.
Oman ilihudumu kama jukwaa la mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu kati ya utawala wa pili wa Trump na Iran Aprili mwaka jana. Tangu wakati huo imefanya awamu kadhaa za mazungumzo kuhusu uendelezaji wa nyuklia wa Iran.