
Waziri wa Usalama wa Iran, Esmail Khatib, ameonya kuwa nchi za Magharibi zitakumbana na madhara ya hatua yao ya kulitaja Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuwa eti ni shirika la kigaidi.
Akizungumza katika kikao cha maadhimisho ya kumbukumbu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Khatib amesema kuwa mataifa ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitoa hifadhi salama kwa makundi ya kigaidi sasa yamechukua hatua ya kuorodhesha IRGC kwenye orodha ya magaidi. Amesema hatua hiyo ya uhasama imechukuliwa katika hali ambayo, ukweli ni kuwa IRGC ni miongoni mwa vikosi madhubuti zaidi duniani katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Kwa hatua ya uhasama, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walitangaza Alhamisi kuwa wamekubaliana kuiweka IRGC kwenye orodha ya kile wanachokiita mashirika ya kigaidi ya umoja huo wa kisiasa na kiuchumi wenye wanachama 27.
Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara mchango wa msingi na muhimu wa IRGC katika kushinda ugaidi katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).
Waziri huyo wa Iran amesisitiza kuwa, “mataifa yanayochukua hatua kama hizi dhidi ya mfumo wetu yanapaswa kuwajibishwa, na bila shaka yatalipa gharama yake.”
Ameongeza kuwa, “uwezo, fahari, subira, jihadi na ujasiri wa Iran vimejengwa na vitaendelea kujengwa juu ya uwepo endelevu wa wananchi katika uwanja wa mapambano; hata hivyo, Magharibi inaendelea kujiongezea udhaifu wake kupitia vitendo hivi vya uhasama.”
Khatib ameashiria maandamano ya hivi karibuni ya umma kote nchini yaliyoonyesha mshikamano wa kitaifa na kusema kuwa taifa la Iran litaendelea kuthibitisha umoja wake na hatimaye kusherehekea ushindi mbele ya vitisho na mashinikizo ya nje.
Maandamano ya Januari 12 yalifanyika kufuatia siku kadhaa za ghasia zilizochochewa na tawala hasimu za kigeni, idadi kubwa ya raia na maafisa wa usalama waliuawa katika mashambulizi ya kigaidi.