Katika mazungumzo aliyoyafanya na Rais wa Marekani Donald Trump, Xi Jinping ameitaka Washington izingatie kuheshimiana katika ushirikiano kati ya pande hizo mbili. Amesisitiza umuhimu wa kujenga uaminifu na kutatua kila changamoto.
Taarifa kutoka serikali ya China zinasema Xi amemuonya Trump alifuatilie suala la Taiwan kwa umakini mkubwa. Kisiwa cha Taiwan ni moja ya masuala nyeti yanayouathiri uhusiano kati ya China na Marekani. Beijing imekuwa ikipinga mauzo ya silaha ya Marekani kwa Taiwan na namna inavyoiunga mkono Taipei.
Kwa upande wake Trump amesema amezungumza na Xi kuhusu masuala ya biashara, vita vya Ukraine na Iran. Amesema pia kuwa China imedhamiria kuongeza kiwango cha manunuzi ya soya ya Marekani kutoka tani milioni 12 msimu uliopita hadi kufikia tani milioni 20 katika msimu huu. Trump amesema mazungumzo hayo ya simu yalikuwa yenye tija na kuwa uhusiano wake na Rais Xi ni mzuri.
China na Urusi zasisitiza ushirikiano zaidi
Katika mazunguzo ya Xi na Rais wa Urusi Vladimir Putin, wawili hao wamezungumzia hali ya kiuchumi ya mataifa yao. Aidha wamesisitiza kuhusu kuimarisha haraka ushirikiano wa nchi zao.
Putin kwa upande wake amesifu namna nchi hizo zilivyotanua ushirikiano wao katika sekta ya nishati, nishati ya nyuklia, teknolojia na utafiti katika masuala ya anga na hatua mpya ya kuondolewa kwa sharti la visa kwa raia wa China na Urusi wanapozitembelea nchi hizo. Msaidizi wa Putin, Yury Ushakov amesema viongozi hao wameizungumzia pia Iran.
Kwa miaka mingi, viongozi wa Ulaya wamekuwa wakiishinikiza China kuacha kuiunga mkono Urusi kutokana na vita vyake nchini Ukraine. Itakumbukwa kuwa kwa sasa, China ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara ikiisaidia Urusi kukabiliana na vikwazo ya mataifa ya Magharibi.