
Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Mediteranean Human Rights Monitor (Euro-Med Monitor) lenye makao yake makuu huko Geneva, Uswisi limekosoa vikali msimamo wa Umoja wa Ulaya kwa kuweka masharti yasiyotekelezeka kwa ajili ya ujenzi mpya wa Gaza.
Katika taarifa ya jana Alkhamisi, Euro-Med Monitor imeonya kwamba, kuoanisha ujenzi mpya wa Gaza na upokonyaji wa silaha za kijeshi kunahalalisha mauaji ya halaiki yanayoendelezwa na Israel dhidi ya watu huko Gaza, sanjari na kukiuka kanuni za msingi za sheria za kimataifa.
Shirika hilo la haki za binadamu limeongeza kuwa, hatua hiyo ni jaribio la makusudi la kupuuza uhalifu mkubwa uliofanywa dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia huko Gaza.
Imesema kwamba, kufungamanisha ujenzi mpya wa Gaza na kufuta harakati za kijeshi kunakiuka kanuni za msingi za sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na majukumu ya kuwalinda raia.
Euro-Med imesisitiza kwamba, Gaza imeharibiwa kabisa tangu kuanza vita vya mauaji ya kimbari vya Israel mnamo Oktoba 2023, huku sehemu kubwa ya uharibifu huo ukiwa dhidi ya miundombinu ya kiraia, nyumba, hospitali, na huduma muhimu.
Kadhalika shirika hilo limelaani vikali matamshi ya hivi karibuni ya Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, ambaye katika matamshi yake ya Januari 29 na Februari 2, 2026, alisema kwamba “ujenzi mpya wa Gaza utategemea kupokonywa silaha wanamapambano wa Hamas.”
Hapo jana pia, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilitangaza kuwa, utawala wa Israel unaendelea kufanya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza, Palestina.