Kampuni ya magari ya Mitsubishi Motors ilipata hasara halisi ya yeni bilioni 4.4, au takriban dola milioni 28 kwa kipindi cha miezi tisa hadi mwezi Desemba mwaka jana, huku ushuru wa forodha wa uagizaji wa Marekani ukiathiri mapato yake.

Kampuni hiyo ya kutengeneza magari ya Japani iliripoti Februari 5 kwamba mauzo ya pamoja yalishuka kwa asilimia 0.6 kutoka mwaka uliotangulia hadi yeni trilioni 1.97 au takriban dola bilioni 12.

Faida ya uendeshaji ilishuka kwa asilimia 69.8 hadi yeni bilioni 31.6, au takriban dola milioni 200.

Kampuni hiyo ilisema hatua za ushuru wa forodha za utawala wa Trump zilipunguza faida ya uendeshaji kwa yeni bilioni 37.3, au takriban dola milioni 238.

Pia ilihusisha utendaji duni na kuyumbayumba kwa kiwango cha ubadilishaji wa fedha.

Lakini kampuni hiyo ya kutengeneza magari ilipitia upya utabiri wake wa mauzo kwa kipindi cha miezi 12 inayoishia mwezi Machi mwaka huu hadi yeni trilioni 2.9, au takriban dola bilioni 18.

Wakati huo huo, kampuni ya Suzuki Motor iliripoti kushuka kwa faida yake ya uendeshaji kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Desemba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mapato ya uendeshaji katika kipindi cha miezi tisa yalipungua kwa asilimia 10.6 hadi yeni bilioni 429.1 au takriban dola bilioni 2.7.

Gharama za malighafi ziliongezeka nchini India ambako Suzuki ina viwanda vingi vya uzalishaji.

Mapato yaliongezeka kwa asilimia 5.4 hadi yeni trilioni 4.51, au takriban dola bilioni 29.

Kampuni hiyo ya kutengeneza magari ilihusisha ongezeko hilo na kupunguzwa kwa ushuru wa bidhaa na huduma nchini India, ambayo ni soko kubwa zaidi la kampuni hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *