
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amezungumzia maadhimisho ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kubainisha kwamba: “katika kipindi hiki, zimefanyika kazi kubwa na adhimu na zimetolewa huduma nyingi ambazo maneno hayatoshi kuzielezea.
Ayatullah Ahmad Khatami amesema, hii kwamba Mapinduzi yameweza kuitoa Iran kwenye utumwa wa Marekani, yenyewe ni jambo la fahari kubwa na kwamba hii leo Iran inaheshimika na inajitawala yenyewe na kuwa na sauti duniani.
Ayatullah Khatami ameashiria pia kuwadia maadhimisho ya harakati adhimu iliyoonyeshwa na askari wa jeshi la anga la Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi na akasema, gwaride la askari hao mbele ya Imamu Khomeini (MA) lilikuwa na taathira kubwa na lilivunja nguvu kuu ya utawala wa kitaghuti.
Ameongeza kuwa, siku ya tarehe 19 Bahman (8 Februari) imesajiliwa katika kalenda ya Iran kwa jina la wapendwa hao wa jeshi la wanaanga, ambao kwa mujibu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wameung’arisha na kuuheshimisha utendaji wa jeshi katika vipindi tofauti, hususan katika kipindi cha vita vya miaka minane vya Kujihami Kutakatifu dhidi ya uvamizi wa utawala wa Iraq ya Saddam.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo jijini Tehran ameashiria machafuko ya uvurugaji amani na umwagaji damu ya hivi karibuni hapa nchini yaliyoratibiwa na kuongozwa na Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel na akasema, katika machafuko hayo, askari waliotumwa na Trump na Netanyahu walichoma moto Misikiti 350, lakini uovu huo uliofanywa na maadui hautaathiri chochote, kwa sababu mahudhurio ya waumini misikitini yamekuwa makubwa zaidi na inshallah wananchi wenyewe watasaidia ili Misikiti izidi kunawiri.
Katika khutba ya kwanza ya Sala ya Ijumaa ya leo, Ayatullah Khatami ameashiria maadhimisho ya kuzaliwa Imamu Mahdi (A’jjalaLlahu Taa’la Farajahu-Ssharif) yaliyofanyika mwezi 15 Shaabani na yanayofahamika na baadhi ya Waislamu kama Siku ya Qasmati-Rizqi na akasema, imani juu ya Umahdi haihusiani na Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee, bali ni itikadi iliyopo kimataifa kwa Waislamu; na zaidi ya hapo ni ya kimataifa kwa wale wote wenye imani ya Mungu mmoja.
Amesema, kimsingi Mashia na Masunni wana mtazamo mmoja juu ya Imamu wa Zama (AS) na akabainisha kwamba, kuwepo kwa Mahdi aliyeahidiwa ni mhimili wa umoja; na si baina ya Shia na Sunni pekee bali kwa wale wote wenye imani ya Tauhidi ya kuwepo Mungu Mmoja pekee wa haki…/