Rais wa China, Xi Jinping, ametoa wito wa kuifanya Renminbi (Yuan), sarafu ya taifa hilo, kuwa sarafu ya akiba ya dunia.
Kwa mujibu wa Pars Today, Xi Jinping amesisitiza umuhimu wa kuigeuza Renminbi kuwa sarafu ya akiba ya kimataifa. Katika kauli zake za hivi karibuni, amesisitiza haja ya kuunda “sarafu yenye nguvu” pamoja na kuimarisha benki kuu ya China na taasisi zake za kifedha za kimataifa, ili China iweze kuwa majukumu makubwa zaidi katika uchumi wa dunia na kushindana na dola ya Marekani.
Kwa mtazamo wake, China inahitaji kuwa na “sarafu imara” itakayoweza “kutumika kwa upana katika biashara za kimataifa, uwekezaji na masoko ya fedha za kigeni, na kufikia hadhi ya sarafu ya akiba.”
Rais wa China kwa muda mrefu amekuwa akijitahidi kuikuza Renminbi katika uwanja wa kimataifa. Hata hivyo, kauli hizi zinaonesha kwa uwazi zaidi maono yake kuhusu lengo la kufikia “sarafu yenye nguvu”, pamoja na kuainisha misingi mipana ya kifedha ambayo Beijing inapaswa kuijenga ili kuiunga mkono.
Xi amesema kuwa misingi hiyo inajumuisha “benki kuu yenye nguvu” yenye uwezo wa kusimamia sera za fedha kwa ufanisi, taasisi za kifedha zenye ushindani wa kimataifa, pamoja na vituo vya kifedha vya kimataifa vinavyoweza “kuvutia mitaji ya dunia na kuathiri upangaji wa bei katika masoko ya kimataifa.”
Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa ikijitahidi kwa dhati kutafuta mbadala wa sarafu ya dola ya Marekani katika ngazi ya dunia, na mojawapo ya mbadala muhimu zaidi ni Renminbi (Yuan). Hatua hii ya China ni matokeo ya mkusanyiko wa sababu za kiuchumi, kisiasa na kimkakati ambazo zimeathiri maamuzi ya kiuchumi ya nchi hiyo.
Sababu ya kwanza kuu ni azma ya China ya kupunguza utegemezi wake kwa dola ya Marekani.
Dola, kama sarafu ya akiba ya dunia, hutumika katika miamala mingi ya kimataifa, ikiwemo biashara ya mafuta na bidhaa nyingine. Utegemezi huu huifanya China kuwa chini ya athari za sera za kiuchumi na vikwazo vya Marekani. China, kama moja ya uchumi mkubwa zaidi duniani, inataka kuubadili mfumo wa kifedha wa dunia ili mamlaka makubwa zaidi yawe mikononi mwa nchi zisizo za Magharibi.
Sababu ya pili ni jitihada za China za kupanua ushawishi wake wa kiuchumi na kisiasa kimataifa. Kupitia miradi kama Mpango wa Ukanda na Njia (Belt and Road Initiative), China inaendeleza uhusiano wa kiuchumi na nchi nyingi. Katika muktadha huu, matumizi ya Renminbi kama sarafu ya miamala katika miradi hiyo yanaweza kuisaidia China kuongeza udhibiti wake juu ya biashara yake ya kimataifa na kupunguza athari ya dola ya Marekani.

Sababu ya tatu inahusiana na uwezo wa kiuchumi wa China na ukuaji wake unaoendelea kuongezeka. China, ikiwa ni uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, sasa ina nguvu ya kutosha kuanzisha sarafu mbadala. Kadiri nguvu zake za kiuchumi zinavyoongezeka, ndivyo inavyoweza kuitambulisha sarafu yake kama sarafu yenye uaminifu katika kiwango cha kimataifa. Nchi nyingi za Asia, Afrika, na hata baadhi ya nchi za Ulaya zinaonesha utayari wa kutumia Renminbi katika biashara za pande mbili, kwani hilo linaweza kupunguza gharama za ubadilishaji wa fedha na pia kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na China.
Vilevile, China inalenga kuilinda mfumo wake wa kifedha dhidi ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani. Endapo Renminbi itakubalika kama sarafu ya kimataifa, hatua hiyo itaiwezesha China kuwa na uimara zaidi mbele ya vikwazo vya kifedha vya Marekani. Kwa sasa, China inaendeleza juhudi kubwa za kuimarisha masoko yake ya kifedha, kuongeza matumizi ya sarafu yake katika miamala ya kimataifa, na kukuza miundombinu ya kifedha inayohusiana na Yuan au Renminbi.
Aidha, kwa kuimarisha sarafu yake katika kiwango cha dunia, China inalenga kubadilisha mfumo wa kifedha wa upande mmoja (unaoegemea sarafu ya dola) na kuanzisha mfumo wa kifedha wa pande nyingi au pande kadhaa. Hatua hii haitakuwa na manufaa kwa China pekee, bali pia kwa nchi nyingine zinazotamani kujinasua kutoka katika utawala wa kibeberu wa sarafu dola katika uchumi wa dunia.
Jambo jingine la kuzingatia ni kwamba kauli za Xi zimetolewa katika kipindi cha kuongezeka kwa hali ya sintofahamu katika masoko ya dunia, hasa baada ya kudhoofika kwa dola ya Marekani. Aidha, mabadiliko katika uongozi wa Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve), pamoja na mvutano wa kijiografia na kibiashara, yamewalazimu magavana wa benki kuu katika nchi mbalimbali kutafakari upya kiwango cha utegemezi wao kwa mali zinazotawaliwa na dola. Hali hii inakuja wakati ambapo wiki iliyopita, kufuatia kauli za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kudhoofika kwa thamani ya dola duniani na madai yake kuwa hali ya dola ni nzuri, sarafu ya Marekani ilifikia kiwango chake cha chini zaidi katika kipindi cha miaka minne iliyopita.