Kulielezea tatizo hili, tunakusimulia maisha ya watu ambao hukaa kwa muda mrefu bila kusimama na madhara wanayoyapata. kila asubuhi, Salim Rashid huwasili ofisini mapema tayari kuanza majukumu yake ya siku. Yeye ni karani katika moja ya ofisi za jiji la Mombasa. Kazi yake kubwa ikiwa ni kukaa mbele ya kompyuta akishughulikia nyaraka mbalimbali.
Kama ilivyo kwa wafanyakazi wengi wa ofisini, Salim hujikuta mara nyingi amekaa kwa muda mrefu bila hata kujitambua, akijitahidi kukamilisha kazi zake kwa wakati Anasema siku ambazo huwa na kazi nyingi, hujikuta akishindwa hata kuinuka kwa sababu huhisi kuwa akisimama atachelewa kumaliza majukumu yake.
” Basi nakaa tu mpaka nimalize. Lakini nikitoka hapo, sasa balaa linaanza,” alisema Salim.
Wataalamu wa afya wanasema mwili wa binadamu haukuumbwa kukaa muda mrefu bila kusogea. Unapokaa kwa saa nyingi; iwe ni ofisini mbele ya kompyuta au nyuma ya usukani, mzunguko wa damu hupungua, hasa kwenye miguu. Hali hii inaweza kusababisha miguu kufa ganzi, kuvimba, au hata kuongeza hatari ya damu kuganda kwenye mishipa.
Madhara mbalimbali ya kiafya
Kukaa kwa muda mrefu pia huathiri sana mgongo na shingo. Wafanyakazi wengi wa ofisini na madereva hulalamika maumivu ya mgongo wa chini, shingo na mabega. Kadri siku zinavyokwenda, maumivu haya yanaweza kuwa ya kudumu na kuathiri uwezo wa mtu kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Patrick Kombe ni daktari katika Hospitali ya Seaside anasema mtu akikaa kwa muda mrefu, kitu cha kwanza kitakachotokea sana ni maumivu ya mgongo, hasa sehemu ya chini karibu na mahali anapokalia. Pili, damu inaweza kuganda kwa sababu haizunguki vizuri, na damu ikiganda inaweza kusababisha miguu kuvimba, na kile kilichoganda kinaweza kusafiri hadi kwenye mapafu au moyo, na hapo mtu anaweza kupata matatizo makubwa kama mshtuko wa moyo au shida ya mapafu.
Lakini madhara hayaishii hapo. Kukaa muda mrefu bila kusogea kunahusishwa pia na kuongezeka kwa uzito kupita kiasi . Mwili hutumia nishati kidogo sana unapokaa, hivyo mafuta huanza kujikusanya polepole. Hivyo, mtu anaweza kupata unene uliopitiliza, ambao huongeza hatari ya shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo.
”Mtu anayekaa sana huwa na kile tunaita slow metabolism. Hii ina maana mwili hauchomi chakula kwa kasi inayotakiwa. Pia mtu anaweza kupata mkao mbaya wa mwili, yaani poor posture. Kwa sababu ya maumivu ya mgongo, hawezi kusimama wima, utaona anatembea akiwa ameinama,” alieleza Daktari huyo.
Madereva pia wanakumbwa na tatizo hili
Kwa madereva hasa, kukaa muda mrefu bila kupumzika husababisha uchovu wa mwili na akili. Uchovu huu hupunguza umakini barabarani na kuongeza hatari ya ajali, jambo linaloweza kuhatarisha maisha ya dereva na watumiaji wengine wa barabara. Mohammed Somobwana, mkazi wa Lamu, ni dereva wa gari dogo anayesafirisha abiria kati ya Lamu na Mombasa. Safari yake huchukua takribani muda wa saa nane hadi tano bila kupumzika.
”Nikiamua kusimama mara kwa mara naona nitachelewa. Lakini nikifika Mombasa, uchovu unakuwa mwingi sana, hasa kiuno kinaniuma. Sina budi kutumia dawa, lakini sasa hilo ndilo limekuwa tatizo langu, ” alisema dereva huyo.
Ili kuepukana na matatizo haya, mtu anashauriwa kuchukua mapumziko ya mara kwa mara, kusimama angalau kila baada ya dakika 30 hadi 60, kufanya mazoezi , kutembea kwa dakika chache na kunyoosha miguu, mikono na mgongo. Pia zingatia kukaa vizuri. Hakikisha kiti kina msaada wa mgongo, miguu inagusa sakafu vizuri, na skrini ya kompyuta iko katika kiwango cha macho.
Hali kadhalika fanya mazoezi hata kama ni madogo, kwani yanasaidia kuboresha mzunguko wa damu na kupunguza madhara ya kukaa muda mrefu. Kumbuka, kukaa muda mrefu bila kusimama ni hatari ya kimya kimya. Haileti maumivu makali mara moja, lakini hujenga matatizo makubwa ya afya kwa muda. Linda afya yako leo kwa kusimama, kusogea na kuujali mwili wako.
