Maelfu ya watu wamejitokeza Ijumaa kwa ajili ya mazishi ya mtoto wa mtawala wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, katika mji ambao bado unaendelea kuonyesha utii kwa kiongozi huyo wa zamani.

Seif al‑Islam Gaddafi, ambaye wakati fulani alionekana na baadhi ya watu kama mrithi mtarajiwa wa Libya, alipigwa risasi na kuuawa nyumbani kwake katika mji wa kaskazini‑magharibi wa Zintan siku ya Jumanne.

Mazishi yake katika mji wa Bani Walid, ulioko takribani kilomita 175 kusini mwa Tripoli, yaliwaleta pamoja maelfu ya wafuasi wa Gaddafi, karibu miaka 15 tangu kiongozi huyo aangushwe na kuuawa katika uasi wa mwaka 2011 ulioungwa mkono na NATO.

Libya imekuwa ikihangaika kurejea kwenye utulivu tangu machafuko hayo. Nchi bado imegawanyika kati ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdelhamid Dbeibah huko Tripoli na serikali ya mashariki inayoungwa mkono na Khalifa Haftar.

Libya -2008-Bango la Muammar al-Gaddafi na mwanae Seif al-Islam
Bango la Muammar al-Gaddafi na mwanae Seif al-Islam Picha: AFP/Getty Images

Dbeibah alilaani mauaji hayo, akisema kuwa “mauaji hayaleti uthabiti… bali huchochea mgawanyiko zaidi.” Wizara yake ya mambo ya ndani ilikuwa imetangaza kuwa itahakikisha “usalama wa mazishi” katika mji huo wenye takriban watu 100,000.

Kila mwaka, Bani Walid huadhimisha kumbukumbu ya mapinduzi ya mwaka 1969 yaliyomleta Gaddafi madarakani, na watu hupita mitaani wakiwa na picha za kiongozi huyo wa zamani na bendera ya kijani ya Libya kabla ya uasi wa Arab Spring.

Kabla ya mazishi siku ya Ijumaa, wakazi pia walibeba picha hizo na bendera huku wakitoa kauli za kumuunga mkono Gaddafi na kutangaza kwamba “damu ya mashujaa haitamwagika bure.”

Marcel Ceccaldi, wakili wa Kifaransa aliyekuwa akimwakilisha Seif al‑Islam, aliambia AFP kuwa “kikosi cha wanaume wanne” kilimuua.

Mamlaka zilisema kwamba zinafanya uchunguzi kuhusu kifo hicho ilhali wauaji bado hawajakamatwa. Saadi Gaddafi, mdogo wake Seif al‑Islam, alisema kaka yake huyo atazikwa “karibu na kaka yake Khamis Gaddafi,” ambaye aliuawa wakati wa machafuko ya 2011.

Chini ya utawala wa miaka 40 wa baba yao uliojaa ukandamizaji, Seif al‑Islam alielezewa kama kiongozi asiyekuwa rasmi, akijijengea taswira ya msimamo wa wastani na mageuzi licha ya kutokuwa na wadhifa wa kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *