Kutokana na juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na wadau zikiwemo za kisera, idadi ya wasichana wanaofanyiwa kitendo hicho imepungua kutoka mmoja kati ya wawili hadi mmoja kati ya watatu duniani ndani ya muongo mmoja uliopita kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Katika siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji wa wasichana na wanawakeinayoadhimishwa Februari 6 ya kila mwaka, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA kupitia taarifa yake ya Februari 3, 2026 limebainisha kuwa zaidi ya wanawake na wasichana milioni 230 wanaishi na madhara ya ukatili huo. Kwa mwaka huu wa 2026, takriban wasichana milioni 4.5 wapo katika hatari ya kukeketwa, huku wengi wao ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Kutokana na mtazamo hasi kuwa mataifa ya kigeni huchochea mapambano dhidi ya ukeketaji ili kuondoa tamaduni za wazawa, siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji wa watoto wa kike na wanawake inapinga mtazamo huu kwa kuonesha jinsi ambavyo, walionusurika, jamii, walimu, wahudumu wa afya, vijana na viongozi wa kidini wanavyosimama kupinga ukeketaji ndani ya jamii zao.
1. Manusura wapaza sauti
Olivia Olivia Albert anaongoza kikundi cha utetezi wa vijana katika mkoa wa Mara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mkoani Mara. nchini Tanzania, ambapo ukeketaji bado unatajwa kuwa wa kiwango kikubwa zaidi, manusura wa ukeketaji wanachukua nafasi za uongozi ili kubadilisha mitazamo kuanzia ngazi ya jamii. Olivia Albert mwenye umri wa miaka 19, ni kielelezo cha mabadiliko baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa ukatili huo akiwa na umri wa miaka 13 pekee, wakati wa likizo kabla ya shule kufunguliwa.
Sasa anaongoza kikundi cha utetezi wa vijana mkoani Mara ambacho kinaendesha vipindi vya elimu shuleni na kufanya kazi na viongozi wa jadi kulinda haki za wasichana walio hatarini.
“Niligundua kuwa sauti yangu ina nguvu. Utetezi kutoka kwa manusura unasaidia kuleta mabadiliko kwenye jamii yangu; wasichana wanaposikia simulizi kutoka kwa mtu aliyeishi katika hali hii, wanasikiliza kwa namna tofauti na wanapata ujasiri.” amesema Olivia.
2. Viongozi wa dini nao washika hatamu
Katika jimbo la Kindia nchini Guinea, Imam Ousmane Yabara Camara Camara ni mtu anayejulikana na kuheshimiwa, na ambaye amechagua kutumia jukwaa lake katika huduma ya wanawake na wasichana wa jamii yake. .
Huko Kindia nchini Guinea, Imam Ousmane Yabara Camara amekuwa sauti muhimu katika kulinda haki za wasichana. Licha ya ukeketaji kuwa haramu nchini humo kwa miaka 20, asilimia 95 ya wanawake walio na zaidi ya umri wa miaka 15 wamefanyiwa ukatili huo. Imam Ousmane Yabara Camara amekuwa akitumia mimbari yake kueleza kuwa ukeketaji si agizo la dini.
“Katika mawaidha yangu, nasema wazi kuwa ukeketaji si amri ya Kiislamu. Wasichana wengi mno wanateseka na madhara makubwa ya kiafya kutokana na kitendo hiki, ni lazima tukikomeshe.” amesema Imam Ousmane.
3. Mataifa yanapitisha sheria kupinga ukeketaji
Huko Djibouti, Nafissa Mahamoud Mouhoumed, Nafissa ni mwanachama wa mtandao wa jamii ‘Elle et Elles’ dhidi ya Ukataji wa Kike.
Mataifa ya Eritrea, Somalia, na Djibouti yamepiga hatua kubwa baada ya wasomi wa Kiislamu kutoa maoni yanayogunduliwa na wanazuoni na kwa kuangalia hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu na mabadiliko ya hali za watu na uhalisia wao, yaani ‘Fatwa’ ya kitaifa mwaka 2025 ikipinga ukeketaji, hatua iliyoambatana na mabadiliko ya Katiba.
Nafissa Mahamoud Mouhoumed kutoka Djibouti ameeleza kuwa sasa wana “ngao mbili” za ulinzi.
“Katika mitaa yetu, sasa tuna ngao mbili zenye nguvu: Katiba na Fatwa. Ushindi huu wa pande mbili unatupa ujasiri wa hali ya juu wa kuziambia familia kuwa imani yako na nchi yako zote zinamlinda binti yako.” Nafissa amebainisha.
4. Wanaume na wavulana ni chachu ya mabadiliko
Katika Eneo la Hadiya la Ethiopia, mzee wa eneo hilo anaongoza mkutano wa kila juma wa kutoa habari na kujadili mazoea mabaya.
Ushiriki wa wanaume na wavulana pia umeonekana kuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko, hususan nchini Ethiopia ambapo asilimia 75 ya wanawake wamefanyiwa ukeketaji. Kupitia programu za UNFPA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, viongozi wa jamii kama Mitiku Gunte wamekuwa wakielimisha wanaume wenzao kuhusu uhusiano wa ukeketaji na matatizo wakati wa uzazi kwa wanwake na wasichana.
Dawit Mohammed, mkulima na mwanaharakati, ameeleza kuwa kuona mifano hai imesaidia wengi kuelewa.
“Mafunzo yametupa zana na ushahidi, hatimaye tumejifunza jinsi ya kuwa na mazungumzo haya magumu na majirani zetu.”
5. Ukeketaji wa kutumia vifaa vya kitabibu
Wafanyakazi wa afya nchini Misri wanahudhuria kampeni ya mafunzo inayoongozwa na UNFPA inayoitwa White Coats Against Female Genital Mutilation.
Wataalamu wa afya wamepewa jukumu la kuzuia “ukeketaji unaotumia vifaa vya kitabibu” ambapo dawa za hospitalini na huduma za afya hutumiwa vibaya kufanya ukatili huo. Nchini Misri, mpango wa “Makoti Meupe dhidi ya Ukeketaji” unawajengea uwezo madaktari kama Maram Mahmoud kuzuia shinikizo la kijamii la kufanya ukeketaji hospitalini.
UNFPA imehitimisha kuwa, katika maadhimisho haya ya leo tarehe 6 Februari, juhudi za pamoja za manusura na jamii ndizo zitakazohakikisha kuwa kila msichana anakua bila hofu ya kufanyiwa ukatili huo wa kimwili na kiakili.