Ukraine na Urusi zimehitimisha duru ya pili ya mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani huko Abu Dhabi siku ya Alhamisi yenye lengo la kuufikisha mwisho mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu vita vikuu vya pili vya dunia, huku pande hizo mbili zikifanya ubadilishaji mkubwa wa wafungwa na kukubaliana kuanza tena mazungumzo hivi karibuni.
Steve Witkoff, mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, alisema wajumbe kutoka Marekani, Ukraine, na Urusi wamekubaliana kubadilishana wafungwa 314 wa vita, jambo ambalo lilifanyika Alhamisi. Ulikuwa ni ubadilishanaji wa kwanza wa wafungwa kama huo katika kipindi cha miezi mitano.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilithibitisha kurudi kwa wanajeshi 157 wa Urusi kutoka utumwani huko Ukraine, pamoja na raia watatu ambao walikuwa wamepelekwa Ukraine wakati wa uvamizi mfupi wa sehemu za eneo la magharibi mwa Urusi la Kursk. Wizara hiyo imesema “Kwa malipo, wanajeshi 157 wa Ukraine waliokamatwa walikabidhiwa.”
Zelenskiy anatarajia duru nyingine ya mazungumzo
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema baadhi ya wafungwa wa vita walioachiliwa huru wameshikiliwa kwa karibu miaka minne. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kiev Zelenskiy alisema duru inayofuata ya mazungumzo itafanyika hivi karibuni, pengine nchini Marekani. Pia alisema, “Ni muhimu kwamba vita hivi vifike mwisho kwa njia ambayo Urusi haipokei zawadi kwa uchokozi wake.”
Witkoff, akiandika kwenye jukwaa la mtandao ya kijamii la X, alisema: “Majadiliano yalikuwa ya kujenga na yalilenga jinsi ya kuunda mazingira ya amani ya kudumu.” Alisema mazungumzo hayo yanaonyesha kwamba ushiriki endelevu wa kidiplomasia unaleta matokeo yanayoonekana na kuendeleza juhudi za kukomesha vita nchini Ukraine.”
Akizungumza katika hotuba yake ya video ya usiku, Zelenskiy alisema Ukraine ilipendelea muundo wowote wa kidiplomasia ambao unaweza kuleta amani karibu zaidi na kuifanya iwe ya kuaminika, ya kudumu, na ambayo inainyima Urusi hamu ya kuendelea kupigana.”
Hapo awali Zelenskiy alisema akiwa pamoja na waziri mkuu wa Poland Donald Tusk, kwamba mazungumzo ya Abu Dhabi yalishughulikia tofauti kuu kati ya pande hizo mbili.
Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine ilisema katika taarifa huku ikithibitisha kwamba mazungumzo hayo yamekamilika, kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu UAE utaendelea na juhudi zake za kidiplomasia na kibinadamu ili kuunga mkono mipango inayolenga kufikia suluhu la amani kwa mzozo nchini Ukraine.”
Marekani na Urusi zakubaliana kufanya mdahalo ya kijeshi
Wakati haya yakiarifiwa Marekani na Urusi zilikubaliana Alhamisi kuanzisha tena mdahalo wa kijeshi wa ngazi ya juu kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka minne katika ishara nyingine ya kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili tangu Rais Donald Trump arudi madarakani na kutaka kukomesha vita nchini Ukraine. Makubaliano hayo yalitokana na mkutano kati ya maafisa wakuu wa jeshi la Urusi na Marekani huko Abu Dhabi.
Mawasiliano ya kijeshi ya ngazi ya juu yalisitishwa mwishoni mwa mwaka wa 2021, huku mvutano kati ya Moscow na Washington ukiongezeka kabla ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.
Kisha Trump akafanya kampeni ya muhula wa pili kwa ahadi kwamba angemaliza mapigano haraka. Mapendekezo yake mengi ya amani yameipendelea sana Kremlin, ikiwa ni pamoja na kuitaka Ukraine kuikabidhi Urusi eneo hilo.
Kamandi ya Marekani barani Ulaya ilisema katika taarifa kwamba njia ya mawasiliano iliyorejeshwa “itatoa mawasiliano thabiti ya kijeshi kati ya pande hizo mbili huku pande hizo zikiendelea kufanya kazi kwa ajili ya amani ya kudumu,”
Jenerali wa Marekani Alexus Grynkewich, ambaye ni kamanda wa vikosi vya Marekani na jumuiya ya kujihami ya NATO barani Ulaya, alikuwa Abu Dhabi, ambapo mazungumzo kati ya maafisa wa Marekani, Urusi na Ukraine kuhusu kukomesha vita yaliingia siku ya pili.
Urusi yaimarisha mashambulizi dhidi ya moundombinu ya nishati ya Ukraine
Wakati huo huo, Urusi iliongeza mashambulizi yake kwenye gridi ya umeme ya Ukraine katika juhudi zinazoonekana kuwanyima raia nishati na kudhoofisha usaidizi wa umma kwa mapigano, huku uhasama ukiendelea katika mstari wa mbele wa vita wa takriban kilomita 1,000 unaopita katika sehemu za mashariki na kusini mwa Ukraine.