Maafisa waandamizi wa Marekani na Iran wanajiandaa kufanya mazungumzo nchini Oman Februari 6 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Swali kuu ni ikiwa duru hii ya mazungumzo itasababisha kupungua kwa mivutano kati ya nchi hizo mbili.
Shirika la Habari la Tasnim la Iran, ambalo lina uhusiano na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lilitoa taarifa kuhusu mazungumzo hayo. Lilisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff watahudhuria.
Mazungumzo hayo yamesitishwa tangu mwezi Juni mwaka jana, wakati jeshi la Marekani lilipofanya mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Shirika hilo la habari lilisema “mada ya mazungumzo hayo si zaidi ya suala la nyuklia na kuondoa vikwazo dhidi ya Iran.” Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema ajenda hiyo inapaswa kujumuisha masuala mengine pia, ikiwa ni pamoja na makombora ya balistiki ya Iran, ufadhili wa mashirika ya kigaidi, na jinsi ya kuwatendea watu wake.
Utawala wa Trump umekuwa ukiongeza shinikizo la kijeshi dhidi ya Iran. Umepeleka meli ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln inayotumia umeme wa nyuklia katika eneo la Bahari ya Arabia karibu na Iran.
Daryl Kimball, mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Kudhibiti Silaha chenye makao yake makuu jijini Washington nchini Marekani amesema kwamba ikiwa wanaweza kukubaliana na “hatua ndogo sana za awali,” inaweza kupunguza mivutano. Alisisitiza kwamba pande zote mbili zinahitaji kuchukua hatua kwa “uhalisia zaidi na utayari wa kubadilika zaidi” ili kuepuka mgogoro mwingine Mashariki ya Kati.