Mbeya. Leo Ijumaa, kuna mechi mbili za Ligi Kuu Bara zinapigwa zikikutanisha timu ambazo hazina matokeo mazuri ziliposhuka dimbani hivi karibuni, hivyo zinatumia kujirekebisha kuona zinapanda kutoka zilipo kwenye msimamo.

Mechi hizo ni Pamba Jiji dhidi ya Coastal Union itakayoanza saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kisha saa 10:15 jioni itakuwa zamu ya Tanzania Prisons dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

 Pamba na Coastal

Wakati kukiwa na tofauti ya pointi sita kati ya Pamba Jiji na Coastal Union katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, timu hizo zinashuka dimbani leo kusaka matokeo ya kuwaweka sehemu nzuri zaidi.

Timu hizo zinazopambana kutoka zilipo na kupanda juu zaidi kwenye msimamo, rekodi zinaonyesha hazina matokeo mazuri sana katika mechi tano zilizopita.

Pamba Jiji yenye pointi 17 ikishika nafasi ya tano baada ya kucheza mechi 12, inaikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa CCM Kirumba uliopo Mwanza.

Katika mechi tano zilizopita, Pamba Jiji imekusanya pointi tano kati ya 15, kufuatia kupokea vichapo viwili dhidi ya JKT Tanzania (3-0) na Mtibwa Sugar (1-0), huku ikiambulia sare mbili dhidi ya Mbeya City (1-1) na Tanzania Prisons (0-0). Pia imeshinda dhidi ya KMC (3-0).

Mechi hiyo itakayopigwa saa 8:00 mchana, Coastal Union yenye pointi 11 ikicheza mechi 12 ikiwa nafasi ya 12, inaingia uwanjani ikiwa haijapata ushindi katika mechi tano za mwisho kwenye ligi, ikiambulia sare mbili dhidi ya TRA United (1-1) na KMC (1-1), huku ikipoteza tatu dhidi ya Namungo (1-0), Azam (3-0) na Yanga (1-0).

Pamba Jiji inayonolewa na Francis Baraza, mara ya mwisho ilipoikaribisha Coastal Union iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, lakini hata hivyo, wapinzani wao hao ni wababe kwani mechi nne walizokutana, Coastal wameshinda mbili, sare moja na Pamba imeshinda moja.

Msimu wa 2020-2021, timu hizo zilikutana katika mechi ya mtoano kuwania kucheza Ligi Kuu Bara 2021-2022. Mechi ya kwanza iliyopigwa Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, ilimalizika kwa sare ya 2-2, ziliporudiana kule Mkwakwani, Tanga, wenyeji Coastal Union walishinda 3-1 na kuzima ndoto za Pamba Jiji kupanda Ligi Kuu.

Lakini msimu wa 2024-2025, Pamba Jiji kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kupita zaidi ya miaka 20, ikaichapa Coastal Union 2-0 pale CCM Kirumba, lakini kabla ya hapo, Coastal iliibuka na ushindi nyumbani wa mabao 2-0.

Kwa takwimu za ligi, timu hizi zimetoshana nguvu, hakuna mbabe kati yao kwani zilipokutana msimu uliopita, kila mmoja alishinda kwake tena kwa matokeo ya 2-2. Leo itakuwaje? Dakika tisini zitaamua.

MATOKEO YAO

Pamba 2-0 Coastal

Coastal 2-0 Pamba

Coastal 3-1 Pamba

Pamba 2-2 Coastal

Prisons, Mashujaa ni vita

Pamoja na kukiri matokeo mabaya iliyopata kikosi chake, Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Zedekiah Otieno, amesema ratiba waliyonayo imechangia kuwaangusha, huku akipigia hesabu za mechi tano zijazo za kufa na mtu kuhakikisha wanajinasua nafasi za chini.

Kuhusu ushambuliaji kuwa butu, kocha huyo raia wa Kenya amesema ameona, akitambia usajili wa nyota Samson Mbangula na George Mpole utaleta mabadiliko makubwa kikosini.

Tanzania Prisons imecheza mechi saba ugenini ikipoteza sita na sare moja, huku nyumbani ikicheza tatu ikishinda moja na sare mbili, inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi nane.

Maafande hao wanaotumia Uwanja wa Sokoine uliopo jiji Mbeya, hivi sasa watakuwa nyumbani kucheza mechi tano mfululizo wakianza leo Ijumaa dhidi ya Mashujaa, Coastal Union (Februari 10, 2026), Namungo (Februari 14, 2026), Simba (Februari 22, 2026) na Azam (Machi 5, 2026), kisha watawafuata KMC (Machi 12, 2026).

Timu hiyo ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja baada ya kushinda mechi zake za play off dhidi ya Fountain Gate, msimu huu imeuanza kwa uchovu ikipoteza mechi sita, sare mbili sawa na ushindi.

Akizungumza na Mwananchi, Otieno amesema kucheza mechi saba kati ya 10 ugenini haikuwa kwenye usawa, hali inayowafanya wachezaji kukosa kucheza kwa uhuru na utulivu.

Amesema kwa sasa wanaporejea nyumbani kuanzia leo dhidi ya Mashujaa wanatarajia kuanza upya kazi kuhakikisha timu inafanya vizuri na makosa yaliyoonekana katika mechi zilizopita amefanyia kazi.

“Kucheza ugenini ndio imetusumbua, tukiwa nyumbani tunakuwa na matokeo mazuri, tumefunga mabao machache, hivyo tunaenda kurekebisha na ujio wa wachezaji wazoefu Mbangula na Mpole wanaweza kuleta mwanzo mpya,” amesema kocha huyo.

Ameongeza kuwa, licha ya kilichowakuta kwa sasa, lakini bado wanaweza kufanya vizuri bila kujali cha ugenini au nyumbani akiahidi kuwa timu inacheza vizuri na kumiliki mpira, hivyo matokeo mazuri yanakuja.

Kwa upande wake nyota wa timu hiyo, Lambart Sabiyanka, amesema bado wanao muda wa kujitafakari na kusahihisha makosa yao akieleza kuwa yaliyotokea msimu uliopita hawatarajii yajitokeze.

Amesema kinachowaangusha kwa sasa ni kutotumia vyema nafasi wanazopata, akieleza kuwa presha kwa wachezaji ni kubwa kutokana na matokeo waliyonayo na kwamba upepo huo utatulia.

“Tumekuwa na mazungumzo wachezaji kuhakikisha tunarudi vizuri uwanjani na kupata matokeo bora, niwatoe hofu mashabiki yaliyojitokeza hayajirudii tena, kimsingi waendelee kutusapoti,” amesema Sabiyanka.

Kwa upande wa Mashujaa, ambayo mechi tano mfululizo haijaonja ushindi ikifungwa tatu na sare mbili, huku ikiruhusu mabao tisa ikiwamo kipigo cha 6-0 dhidi ya Yanga, kisha 2-0 na Simba na 1-0 mbele ya KMC, leo ina kazi ya kujiuliza mbele ya Prisons.

Matokeo hayo ya kukosa ushindi katika mechi tano mfululizo yameonekana kuwaumiza Mashujaa, huku benchi la ufundi likitoa msimamo kwa nyota wake na kuahidi kurejesha kasi waliyoanza nayo msimu huu.

Huu ukiwa ni msimu wa tatu Mashujaa inashiriki Ligi Kuu, ilikuwa na mwanzo mzuri msimu huu hadi kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu kabla ya mambo kuwaharibikia na kujikuta nafasi ya 10 kwa pointi 13.

Katika mechi tano za mwisho, timu hiyo haijaonja ushindi wowote, ikiwa ni kupoteza tatu kwa kuruhusu mabao tisa na sare mbili huku ikiambulia patupu bila bao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa Mashujaa, Charles Fredi, amesema mechi zilizopita wamepata matokeo mabaya na mwenendo si mzuri akieleza kuwa hali hiyo inawaumiza wote ndani na nje ya timu.

Amesema baada ya matokeo hayo, wamekaa na kutafakari walipokosea, hivyo kuanzia mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons leo Ijumaa wanaamini watarejesha ubora wao na kasi waliyoanza nayo msimu.

“Imetuumiza wote, matokeo si mazuri na mwenendo ni mbaya ila tumeona tulipokosea na kuanzia mchezo wa kesho dhidi ya Prisons tunahitaji ushindi ili kurekebisha makosa na kufanya vizuri,” amesema kocha huyo.

Kwa upande wake straika wa timu hiyo, Chrispin Ngushi, amesema wamekuwa na ubutu kwenye kufunga mabao, lakini mazoezi waliyofanya anaamini Mashujaa itarejesha upya makali yake.

“Tumekuwa tunapata nafasi za mabao tunashindwa kutumia vyema, sisi washambuliaji kiu na kilio chetu ni kuona tunaipa matokeo mazuri timu na tunaahidi mechi ijayo tutaanza upya,” amesema nyota huyo.

Rekodi zinaonyesha, zinapokutana Tanzania Prisons na Mashujaa, ni mechi moja pekee nyavu hazikutikiswa zilipotoka 0-0 (Agosti 23, 2024) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Katika mechi nne za Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo, Prisons imeshinda mbili, Mashujaa imeshinda moja, sare ikiwa moja, huku yakifungwa jumla ya mabao manane. Jambo zuri ni kwamba, kila mmoja amewahi kumfunga mwenzake akiwa ugenini.

Prisons 2-1 Mashujaa

Mashujaa 0-0 Prisons

Prisons 1-2 Mashujaa

Mashujaa 0-2 Prisons

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *