
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya shirika la kimataifa la ufuatiliaji wa njaa, Integrated Food Security Phase Classification, maarufu kama IPC, njaa sasa imeathiri miji miwili zaidi ya Umm Baru na Kernoi katika eneo la Darfur. Hii ni baada ya shirika hilo kuthibitisha mwaka jana kuwa wakazi wa mji mkubwa wa el-Fasher walikuwa tayari wanakabiliwa na njaa kufuatia mzingiro wa miezi 18 na makundi ya wapiganaji.
Tangu Aprili mwaka 2023, Sudan imekumbwa na vita vikubwa baada ya mvutano wa madaraka kati ya jeshi la taifa na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces, RSF. Umoja wa Mataifa umeutaja mzozo huo kuwa ndio mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani kwa sasa.
Ripoti ya IPC imetolewa wakati kundi la RSF likiripotiwa kufanya shambulio dhidi ya hospitali ya kijeshi katika mji wa Kouik, kusini mwa jimbo la Kordofan, na kusababisha vifo vya watu 22, akiwemo mkurugenzi wa hospitali hiyo na wahudumu wengine wa afya. Watu wanane walijeruhiwa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa mtandao wa madaktari wa Sudan unaofuatilia matukio ya vita.
Mtandao huo umeeleza kuwa mashambulio dhidi ya vituo vya afya si tukio la pekee, bali ni sehemu ya mashambulizi ya mara kwa mara yaliyosababisha hospitali kadhaa kushindwa kutoa huduma.
Takwimu za Umoja wa Mataifa
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu elfu 40 wameuawa tangu vita kuanza, huku zaidi ya watu milioni 14 wakilazimika kuyahama makazi yao. Hata hivyo, mashirika ya misaada yanasema idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa ripoti ya IPC, hali ya njaa imegunduliwa rasmi katika miji ya Umm Baru na Kernoi. Takwimu zinaonesha kuwa karibu asilimia 53 ya watoto wenye umri wa kati ya miezi sita na miaka mitano mjini Umm Baru wanakabiliwa na utapiamlo mkali, huku asilimia 32 ya watoto mjini Kernoi wakipitia hali hiyo hiyo.
Ripoti hiyo imeonya kuwa viwango hivyo vya utapiamlo vinaongeza hatari ya vifo na vinaashiria kuwa maeneo jirani huenda pia yanakabiliwa na hali mbaya sawa na hiyo.
Kuanguka kwa mji wa el-Fasher mikononi mwa RSF mwishoni mwa mwaka 2025 kulisababisha wakazi wengi kukimbilia miji ya jirani, jambo lililoongeza shinikizo kwa rasilimali chache na kuongeza tatizo la uhaba wa chakula.
Kwa sasa, idadi ya maeneo yaliyothibitishwa kukumbwa na njaa nchini Sudan imefikia tisa. Mwaka 2024, njaa iliripotiwa katika maeneo kadhaa ya Darfur Kaskazini na katika eneo la Milima ya Nuba.
Ripoti hiyo pia imeonya kuwa maeneo ya Kordofan yako katika hatari ya kukumbwa na njaa kali zaidi, kutokana na kusambaratika kwa uzalishaji wa chakula na njia za usambazaji, hasa katika miji iliyozingirwa na maeneo yaliyotengwa.
Wataalamu wanasema njaa hutangazwa rasmi pale vifo vinavyotokana na utapiamlo vinapofikia angalau watu wawili kwa kila watu elfu kumi, au watoto wanne chini ya umri wa miaka mitano, huku zaidi ya asilimia 30 ya watoto wakikabiliwa na utapiamlo mkali.