Rais wa Jamhuri ya Kongo (Brazzaville), Denis Sassou Nguesso, ametangaza kwamba atagombea tena urais wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Machi, akiwa na lengo la kusalia madarakani kwa zaidi ya miongo minne huku akiwa na umri wa miaka 82.

“Nitashiriki kama mgombea katika uchaguzi wa urais,” alisema kiongozi huyo jana Alkhamisi kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Nguesso alitangaza azma yake mbele ya umati wa maelfu ya watu katika wilaya ya kusini ya Ignie.

Kisheria, Nguesso hana kizuizi cha kushiriki katika kinyang’anyiro hicho kwa sababu marekebisho ya katiba yaliyopitishwa mwaka 2015 yameondoa kizuizi cha umri kilichokuwa kimewekwa huko nyuma cha miaka 70 kwa wagombea urais na kuanzisha mfumo wa mihula mitatu ya miaka mitano.

Rais Nguesso ameiongoza Jamhuri ya Kongo, inayojulikana pia kama Kongo-Brazzaville, katika mfumo wa chama kimoja tangu mwaka 1979 hadi 1992, kabla ya kushindwa na Pascal Lissouba katika uchaguzi wa kidemokrasia wa kwanza. Alirudi tena madarakani mwaka wa 1997 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, na amekuwa akiongoza nchi hiyo tangu wakati huo hadi sasa.

Chama tawala Congolese Labour Party (PCT) kilitangaza mwezi Disemba mwaka jana kwamba kiongozi huyo atawania urais kwa muhula mwingine mpya.

Kwa mara ya mwisho Nguesso alitangazwa tena mshindi katika uchaguzi wa urais wa Machi 2021 kwa kupata zaidi ya asilimia 88 ya kura…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *