
Wataalamu wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa walionya Alhamisi kwamba njaa inaenea katika eneo la magharibi mwa Darfur la Sudan, huku vita kati ya jeshi na vikosi vya wapiganaji vikiacha mamilioni wakiwa na njaa, wakimbizi wa ndani na kukatizwa misaada.
Tangu Aprili 2023, mgogoro kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa kundi la RSF umewaua maelfu ya watu, ukiwalazimisha watu milioni 11 kuyahama makazi yao na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mojawapo ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Katika tahadhari iliyotolewa na Shirika linalofuatilia masuala ya usalama wa upatikanaji wa chakula IPC, wataalam wa usalama wa chakula duniani walisema kwamba “viwango vya njaa kwa utapiamlo mkali sasa vimepitwa” katika maeneo yanayogombaniwa ya Um Baru na Kernoi Kaskazini mwa Darfur, karibu na mpaka na Chad.
Wataalamu wa shirika hilo pia wamesema viwango hivi vya kutisha vinaonyesha hatari kubwa ya vifo vingi na kuongeza wasiwasi kwamba maeneo ya karibu yanaweza kuwa yanakabiliwa na hali kama hizo za janga.