
Dar es Salaam. Mwaka 1996, katikati ya changamoto za kiafya na rasilimali chache, wazo lilizaliwa la kuanzisha hospitali maalumu kwa wagonjwa wa saratani. Hivyo, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ilianzishwa chini ya Sheria ya Bunge, kwa dhamira ya kuhudumia maisha ya watu.
Mpaka sasa ORCI imeikisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake na katika maadhimisha hayo kutafanyika kongamano la kwanza la kimataifa la saratani na uzinduzi wa tovuti maalumu.
Dk Diwan Msema, Mkurugenzi wa ORCI, anasema mwanzo haukuwa rahisi, lakini taasisi ilianza safari yake kwa unyenyekevu na dhamira isiyotikisika ya kuhudumia wananchi na kuokoa maisha. “Miaka imeendelea, taasisi imejifunza, kujipanua na kujijenga ili kukidhi mahitaji yanayobadilika ya jamii,” anasema.
Anaeleza mafanikio makubwa yametokana na uwekezaji wa Serikali, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliwekeza zaidi ya Sh40 milioni kuboresha miundombinu ya matibabu. Pia, Serikali iliunda mpango mkakati wa miaka 10 wa kudhibiti saratani, uliomalizika mwaka juzi.
Anasema maboresho hayo ya Serikali yamesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi tofauti na zamani ambapo wote walilazimika kutibiwa ORCI. “Februari 12 na 13 mwaka huu tunapoadhimisha miaka 30 ya kuwepo kwa hospitali hii hakuna haja ya wagonjwa kwenda India, kila kitu kinawezekana ndani ya ORCI. Hali hiyo imewezesha kupunguza utegemezi kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali nyingine.”
Akizungumzia maadhimisho hayo, Daktari mstaafu Khamza Maunda anasema awali hawakuwa na vifaa na wafanyakazi wa kutosha, lakini walijijenga taratibu. Kati ya 2013-2018, taasisi ilianzisha masomo ya kufundisha madaktari kuwa mabingwa wa saratani hatua hii ilikuwa msaada mkubwa kwa taasisi.
Dk Yokebeth Vuhahula anasema walikuwa hawana Idara ya radiolojia muhimu kugundua saratani, lakini sasa vipimo vinapatikana hospitalini.
Mmmoja wa wagonjwa waliopambana na saratani na kupona, Babu wa Kitaa anasema ORCI ni tofauti, wagonjwa waliopona wanashiriki vikao vya kujadili saratani. “Mbali na kutibiwa ukipona unakuwa sehemu ya mafanikio ya hospitali, hili kangu ni taofauti kwani wagonjwa tuliopona tunahudhuria vikao vya kujadili maradhi haya.”
Dk Carol Swai anabainisha kuwa uwekezaji wa Serikali umesaidia hospitali kupokea wagonjwa wengi kutoka nchi jirani na utoaji wa huduma rafiki na yenye ukaribu.
Safari ya ORCI inaonyesha jinsi maono, uwekezaji wa Serikali, na bidii ya wataalamu yameweza kuboresha matibabu ya saratani nchini. “Miaka 30 ya ORCI ni ushahidi wa ujasiri, dhamira na mafanikio katika kuokoa maisha ya wagonjwa,”Dk Msema.