Msemaji wa jeshi la polisi Taqi Jawad ameliambia shirika la habari la DPA kwamba mshambuliaji alitembea kwa miguu hadi karibu na eneo la msikiti na kuanza kuwafyatulia risasi walinzi waliokuwa kwenye lango kuu la kuingilia na hatimaye kuingia msikitini.
Jawad, aliyenukuu ripoti za awali kulingana na mashuhuda amesema mshambuliaji huyo kisha aliingia msikitini na kufyatua mabomu aliyokuwa ameyafunga kwenye fulana yake na kusababisha vifo na majeruhi.
Baba wa Own Shah ni miongoni mwa majeruhi wa shambulizi hilo kama anavyosema, “Baba yangu amejeruhiwa vibaya sana, mguu wake umejeruhiwa na amepata tundu tumboni. Tunaishi hapa Tarlai, nilikuwa nyumbani kwangu, ninaumwa. Vinginevyo mimi na kaka yangu tungekuwa pia msikitini. Sisi, sote watatu, hatukuwa tunajisikia vizuri, ndiyo maana tulikuwa nyumbani. Baba alikuja kwa ajili ya sala ya Ijumaa, tulisikia mlipuko na mama akaniambia huu ulikuwa mlipuko wa aina gani?”
Afisa mmoja mwandamizi wa eneo hilo Irfan Memon amesema wanaweza kuthibitisha vifo 31 hadi sasa, lakini wanahofia kwamba idadi hiyo itaongezeka kwa sababu wengi wa waliojeruhiwa, wana hali mbaya mno. Kikosi cha waokozi waliwapeleka zaidi ya majeruhi 150 hadi kwenye hospitali kuu ya Islamabad ambako hali ya tahadhari ilitangazwa.
Tamko la serikali
Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif wamelaani shambulizi hilo kwenye taarifa tofauti na kutuma salamu za pole kwa familia za wahanga. Waziri Mkuu Shehbaz kwa upande wake ameziagiza mamlaka kuwapatia huduma bora kabisa majeruhi hao na kutaka kufanyike uchunguzi.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo, lakini kuna mashaka makubwa kwamba makundi ya wanamgambo kama ya Taliban wa Pakistan au lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS, ambayo yalishutumiwa kwa mashambulizi ya huko nyuma dhidi ya waumini wa Kishia, ambao ni wachache nchini humo wapatao asilimia 20, kati ya idadi jumla ya watu milioni 250.
Shambulizi kubwa la mwisho mjini Islamabad lilitokea mwaka 2008, baada ya mshambuliaji wa kujitoa muhanga kuilenga Hoteli ya Marriot na kuwaua watu 63 na wengine 250 walijeruhiwa.
Mashambulizi yanayofanywa na wanamgambo hao wa Kiislamu yameongezeka nchini Pakistan tangu Taliban waliporejesha udhibiti wa taifa jirani la Afghanistan. Kundi la Taliban la Pakistan, ambalo ni tofauti na lile linalotawala Afghanistan nalo linashutumiwa kwa kufanya operesheni zake kwenye eneo la mpaka na linahusishwa na visa kadhaa vya kuvishambulia kwa mabomu vikosi vya usalama pamoja na raia.