Mchezo wa fainali wa Ligi ya Mpira wa Miguu Marekani (NFL) wa Super Bowl mwaka huu, unazikutanisha Seattle Seahawks na New England Patriots, lakini bado haijulikani ikiwa mchezo huo mkubwa utawapumzisha Wamarekani kutoka kwenye mazingira mazito ya kisiasa.
Mchezaji wa Seahawks Cooper Kupp anaamini kuwa angalau kwa saa chache, taifa linaweza kuungana kupitia mchezo huo.
Super Bowl ni nini?
Super Bowl ni mchezo wa fainali wa Ligi ya Mpira wa Miguu wa Marekani maarufu NFL. Ni tukio kubwa la kitaifa Marekani linalojulikana kwa maonyesho ya muziki wakati wa mapumziko, Matangazo ya biashara ya gharama kubwa, sherehe, burudani na hafla mbalimbali.
Mchezo huo umejizolea umaarufu na utazamaji mkubwa zaidi wa mamilioni ya watu ndani na nje ya Marekani. Mwaka jana, mcehzo wa fainali wa Super Bowl kati ya Philadelphia Eagles vs. Kansas City Chiefs ulitazamwa na watazamaji wastani wa milioni 127.7 nchini Marekani, idadi ambayo iliweka rekodi mpya ya watazamaji wengi zaidi katika historia ya televisheni ya Marekani. Aidha, idadi ya juu zaidi ilifikia takribani milioni 137.7 wakati wa robo ya pili ya mchezo.
Mivutano ya kisiasa katika burudani
Rais wa Marekani Donald Trump hatahudhuria mchezo huo, lakini kwa muda mrefu Super Bowl imekuwa zaidi ya mpira na burudani.
Mvutano wa kisiasa unaendelea kuigubika Super Bowl ya mwaka huu, huku utawala wa Rais Donald Trump ukiendelea kugonga vichwa vya habari—safari hii kutokana na msukumo wake mkali wa kutaka Marekani idhibiti Greenland pamoja na utekelezaji wa sera kali za uhamiaji zinazoongozwa na ICE.
Kundi hilo limekuwa likitekeleza oparesheni katika miji mbalimbali, na mapema Januari maafisa wa shirikisho waliwaua kwa risasi raia wawili wa Marekani nchini Minneapolis, tukio lililozidisha hasira na hofu miongoni mwa wananchi. “Ni huzuni kwamba tumefika hapa kama taifa,” amesema mchezaji Cooper Kupp.
Mvutano huo pia umejitokeza katika eneo la burudani, baada ya Trump kumshambulia Bad Bunny msanii atakayetumbuza wakati wa mapumziko akimtaja kama “chaguo baya.”
Msanii huyo wa Amerika ya Kusini, ambaye huimba kwa Kihispania pekee, amekuwa akikosoa sera za Trump za uhamiaji, na alishinda Tuzo za Grammys wiki iliyopita na kusema kwamba, “sisi si wakatili, si wanyama, si wageni, sisi ni binadamu na sisi ni Wamarekani.”
Katika msimu ambao wengi walitarajia mchezo ungeleta unafuu, masuala ya kisiasa yanaendelea kuingia katikati ya Super Bowl—hata hivyo Kupp bado anaamini kuwa angalau kwa muda mfupi, mpira unaweza kuwaleta watu pamoja.
Super Bowl ya mwaka huu itafanyika siku ya Jumapili, tarehe 8 Februari 2026.