
Tabora. Serikali ya Mkoa wa Tabora imepokea vifaa vya kufanyia tathmini ya hali ya lishe kwa vijana rika balehe wenye umri wa miaka 10 hadi 19, vyenye thamani ya zaidi ya Sh25 milioni, kwa lengo la kuboresha huduma za lishe na afya kwa kundi hilo.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa jana, Februari 5, 2026, na Mradi wa Kuboresha Afya ya Wasichana kwa Kuzingatia Misingi ya Haki (BRIGHT), kufuatia ombi la Serikali ya Mkoa wa Tabora la kupata nyenzo zitakazowezesha tathmini ya kina ya hali ya lishe kwa vijana.
Imeelezwa kuwa tathmini hiyo itachangia kuongeza ufanisi na usahihi katika utoaji wa huduma za lishe kwa wasichana na wavulana rika balehe, pamoja na kuwezesha ugunduzi wa mapema wa tatizo la utapiamlo ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mradi wa BRIGHT mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Emiliana Maswi alisema mradi huo, unaofadhiliwa na Serikali ya Canada, utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ikiwamo utoaji wa vifaa vya tathmini.
“Mkurugenzi ambaye namwakilisha amesema tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania, hususan Mkoa wa Tabora, ili kuhakikisha vijana wanakua wakiwa na afya bora, hasa katika rika hili nyeti la balehe,” amesema Maswi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora anayesimamia Idara ya Ukaguzi na Ufuatiliaji, Amosi Kim, alisema vifaa hivyo vitaleta tija kubwa kwa kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za afya za vijana na kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa.
“Wakati mwingine changamoto hushindikana kupatiwa ufumbuzi wa mapema kwa sababu tathmini haijafanyika kwa kina. Vifaa hivi vitatusaidia kupata takwimu sahihi na kutoa suluhisho sahihi,” amesema Kim.
Hata hivyo, Kim ameomba ushirikiano huo kuendelezwa akibainisha kuwa zoezi la tathmini ya lishe ni endelevu kutokana na ongezeko la vijana siku hadi siku.
“Watoto wanazaliwa kila siku, hivyo kundi la vijana linaongezeka. Ni lazima tathmini ifanyike mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto za lishe mkoani Tabora,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa elimu ya lishe, mkazi wa Tabora na kijana mwenye umri wa miaka 19, Yasini Ndoriki, amesema jamii inapaswa kuelimishwa kuwa lishe bora haimaanishi vyakula vya gharama kubwa.
“Mazingira yetu yana chakula cha kutosha; tunafuga kuku, tuna mayai, nyama na mboga za kutosha. Lishe bora ni mpangilio wa chakula, si utajiri,” amesema Ndoriki.
Naye Asia Ramadhani (17), mkazi wa Tabora, aliomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kubadili dhana potofu kuwa lishe bora ni vyakula vya gharama.
“Wengi tunadhani lishe bora ni nyama, mayai au vyakula vya bei kubwa kama pizza, kumbe ni vyakula vya kawaida vinavyotuzunguka. Elimu itusaidie kuelewa hilo,” alisema.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto Tanzania (TDHS) wa mwaka 2015/2016, Mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya pili nchini kwa kiwango cha wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 walioanza kuzaa, kwa asilimia 43.
Aidha, utafiti wa mwaka 2022 unaonyesha Tabora ilishika nafasi ya tatu kwa kiwango cha juu cha ukatili wa kijinsia, ambapo asilimia 48 ya wanawake walioolewa au waliowahi kuolewa wenye umri wa miaka 15 hadi 49 waliripoti kuathiriwa na ukatili wa kimwili, kingono au kisaikolojia kutoka kwa wenza wao.