
Rais wa Marekani, Donald Trump amepinga pendekezo la Rais wa Russia, Vladimir Putin la kuongezwa kwa khiari muda wa Mkataba wa New START, unaoweka mipaka ya silaha za nyuklia, ambao muda wake ulimalizika jana Alkhamisi.
Trump alisema Alkhamisi kwamba, anataka wapatanishi kutoka nchi zote mbili waketi chini pamoja na kusaini makubaliano mapya, akiuita wa sasa mkataba wa zamani “uliojadiliwa vibaya”.
“Badala ya kurefusha muda wa ‘New START’ (Mkataba uliojadiliwa vibaya na Marekani ambao, mbali na kitu kingine, unakiukwa vikali), tunapaswa kuwa na Wataalamu wetu wa Nyuklia wafanyie kazi Mkataba mpya, ulioboreshwa, na wa kisasa ambao unaweza kudumu kwa muda mrefu katika siku zijazo,” Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.
Huko nyuma, Trump alisema kwamba angependa China ihusishwe katika mkataba huo mpya, lakini mamlaka za Beijing hazijaonyesha nia ya kufanya hivyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa, Mkataba wa New START, ulimalizika rasmi jana Februari 5, na kwamba hadi sasa Moscow haijapokea jibu lolote rasmi kutoka kwa Washington kuhusu kuuongezea muda mpya mkataba huo.
Kumalizika muda wa mkataba wa New START kunayaacha madola hayo mawili makubwa yenye silaha za nyuklia bila uangalizi wowote za silaha hizo hatari.
Mkataba wa New START, ambao ulisainiwa mwaka 2010 na kurefushwa mwaka 2021, unaweka mipaka ya vichwa vya nyuklia vya makombora na mitambo ya makombora hayo ya kimkakati na kuweka mifumo ya usimamizi wa silaha hizo za Russia na Marekani.