Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito wa mkataba mpya kufuatia kumalizika muda kwa mkataba wa kudhibiti silaha za nyuklia wa New START na Urusi.

Trump alisema katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii Februari 5 kwamba badala ya kuongeza muda wa Mkataba wa Kupunguza Silaha za Kimkakati au New START, “tunapaswa kuwa na Wataalamu wetu wa Nyuklia kufanyia kazi Mkataba mpya, ulioboreshwa, na wa kisasa ambao unaweza kudumu kwa muda mrefu katika siku zijazo.”

Mkataba wa New START ulikuwa wa mwisho uliosalia kuhusu kupunguza silaha za nyuklia kati ya Marekani na Urusi. Uliweka ukomo wa idadi ya vichwa vya nyuklia vya kimkakati vinavyowekwa tayari kuwa 1,550.

Rais wa Urusi Vladimir Putin mwezi Septemba mwaka jana kimsingi alipendekeza muda wa mkataba huo kuongezwa kwa mwaka mwingine mmoja. Lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa na Marekani, na mkataba huo ulimalizika Februari 5.

Alipoulizwa kama kuna makubaliano ya muda na Urusi ya kuzingatia masharti ya mkataba wa New START, Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt alisema, “Sifahamu chochote.”

Trump ameashiria kuwa makubaliano yoyote ya siku za usoni ya udhibiti wa silaha za nyuklia yanapaswa kuijumuisha China, ambayo inasemekana kupanua uwezo wake wa nyuklia kwa kasi.

Ikiwa mkataba mpya utajadiliwa, mpangokazi wake unatarajiwa kuwa suala muhimu, pamoja na ukomo wa silaha za nyuklia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *