
Hatua hiyo inaleta “hatari kubwa ya kibinadamu” kwa raia wanaoishi katika maeneo hayo, imesisitiza Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa OHCHR, wakati ikitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Geneva.
“Matumizi ya viua-magugu yanaibua maswali kuhusu athari zake kwa ardhi za kilimo za eneo hilo na jinsi hali hiyo itakavyoathiri kurejea kwa raia makwao na katika maisha yao ya kujikimu kwa muda mrefu,” amesema Alessandra Vellucci, Mkurugenzi wa Huduma ya Habari ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva.
Akirejea kauli iliyotolewa jana Alhamisi na Msemaji wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Bi. Vellucci amesisitiza wajibu wa pande zote chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.
“Shughuli yoyote ya Jeshi la Ulinzi la Israel IDF, inayofanyika kaskazini mwa Mstari wa Bluu ni ukiukaji wa azimio namba 1701,” amewaambia waandishi wa habari.
Msemaji wa OHCHR, Thameen Al-Kheetan, amsisitiza kuwa taarifa hizo zinahitaji uchunguzi wa kina zaidi “ili kuthibitisha aina ya kemikali zilizotumika. Mashambulizi dhidi ya mashamba na vyanzo vya maji yanaleta hatari kubwa ya kibinadamu,” amesema.
Onyo kuhusu Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu
Afisa huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa pia ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayoendelea katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu, akionya kuwa operesheni mpya za kijeshi za Israel na upanuzi wa makazi zinaweka hatarini uwezekano wa kuundwa kwa dola ya Palestina inayoweza kuishi.
Tangu mwaka jana, makumi ya maelfu ya Wapalestina wamelazimika kuyahama makazi yao kwa nguvu katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.
Hii inajumuisha kambi tatu za wakimbizi zilizoathiriwa na operesheni ya kijeshi ya Israel iitwayo “Iron Wall”, ambayo iliwang’oa zaidi ya watu 32,000 kutoka kambi za Jenin, Tulkarem na Nur Shams.
Kwa mujibu wa Bwana. Al-Kheetan, wakazi hao bado hawajaweza kurejea nyumbani, na nyumba nyingi zimeharibiwa na majeshi ya Israel.
Operesheni mpya za kiusalama za Israel zinazoathiri Wapalestina pia zimejumuisha kampeni katika Yerusalem Mashariki inayokaliwa kimabavu, zikiwemo angalau operesheni mbili kubwa zilizolenga jamii mbili za Kipalestina, kulingana na OHCHR.
“Katika kambi ya wakimbizi ya Shu’fat, walivamia nyumba na maduka kadhaa, kuwakamata angalau Wapalestina 25, kunyang’anya mali na kukamata magari binafsi 10,” ameeleza Bw. Al-Kheetan.
“Katika operesheni nyingine kubwa, iliyolenga eneo la Kafr Aqab na mipaka ya kambi ya wakimbizi ya Qalandiya, majeshi ya usalama ya Israel yanaripotiwa kubomoa majengo 70 ya Wapalestina. Inaonekana hatua hiyo ni maandalizi ya miradi mikubwa ya makazi katika eneo hilo.”
Haya yote yanaongezeka juu ya “vurugu zisizokoma za walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina kwa msaada na ushiriki wa majeshi ya usalama ya Israel”, imesema OHCHR, ikiongeza kuwa makazi ya Israel yanaendelea kupanuka “kwa kasi kisichowahi kushuhudiwa kinyume na sheria za kimataifa.”
OHCHR imesema kuwa mwezi Desemba, mamlaka za Israel ziliomba zabuni za ujenzi wa zaidi ya nyumba 3,000 za makazi katika eneo lililo kati ya vituo vitatu vikubwa vya miji ya Wapalestina, Jerusalem Mashariki, Ramallah na Bethlehem.
Akijibu swali kuhusu mpango wa Israel unaoitwa “E1”, ambao unaripotiwa kutenganisha Ukingo wa Magharibi wa kaskazini na kusini na Yerusalem Mashariki, Bwana. Al-Kheetan ameonya kuwa mpango huo “una hatari ya kutenganisha jamii za Wapalestina na kuathiri kwa kiwango kikubwa uwezekano wa kuundwa kwa dola ya Palestina.” Amesisitiza kuwa, “msingi wa suala ni kwamba makazi yote lazima yaondolewe na shughuli zote za ujenzi wa makazi zikomeshwe.”