Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu kile ulichokielezea kama ongezeko la vitishio vya kundi la Daesh (ISIS) tangu katikati ya mwaka jana, ukieleza kuwa kundi hilo limekuwa “tata zaidi”.

Katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi, Alexander Zuev, amesema kwamba Daesh na washirika wake wamepanua uwepo wao Afrika Magharibi na eneo la Sahel, na wanaendelea kufanya mashambulizi katika nchi za Iraq na Syria.

Kwa mujibu wa Zuev, kuondolewa kwa vikosi vya Syrian Democratic Forces (SDF) katika kambi ya al-Hol kaskazini mashariki mwa Syria mnamo Januari 21 kumesababisha changamoto mpya za kiutendaji na kibinadamu.

Kambi hiyo inahifadhi takriban watu 24,000, wakiwemo karibu Wasyria 15,000, na wanawake na watoto wa kigeni 6,300 wa mataifa 42, ambao nchi zao zinakataa kuwapokea tena.

Zuev ametahadharisha kwamba “kundi la Daesh na matawi yake limeendelea kubadilika na kuonyesha ustahimilivu licha ya mashinikizo yanaloendelea ya kupambana na ugaidi.”

Afisa huyo wa UN ameongeza kuwa: “Nchini Afghanistan, Daesh inasalia kuwa moja ya vitisho vikubwa zaidi katika Mkoa wa Khorasan na kwingineko.”

Ameeleza kuwa shambulio la kutumia silaha kwenye Ufuo wa Bondi nchini Australia mwezi Desemba mwaka jana, ambalo lilisababisha vifo vya watu 15, “lilichochewa na itikadi ya kundi hilo.”

Mwezi uliopita pia, kundi hilo lilidai kuhusika na shambulio lililolenga uwanja mkuu wa ndege nchini Niger.

Kwa upande wake, mkuu wa Kurugenzi ya Utendaji ya Kamati ya Kupambana na Ugaidi ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa kundi la Daesh inasasisha mbinu zake, na kuongeza: “Wamepanua matumizi yao ya mali pepe (virtual assets), ikiwa ni pamoja na sarafu za kidijitali na zana za intaneti, mifumo ya ndege zisizo na rubani na utumiaji wa akili mnemba.”

Amesema Daesh inazidi kutumia akili mnemba kukuza “ugaidi na uandikishaji wa magaidi, likiwalenga vijana na watoto.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *