Merz ameyasema haya wakati ambapo Urusi inaituhumu Ukraine kuhusiana na jaribio la mauaji dhidi ya jenerali wake wa ujasusi.

Akizungumza wakati alipokuwa akikamilisha ziara yake ya siku tatu katika eneo la Ghuba, Kansela Merz amesema Ulaya siku zote iko tayari kwa mazungumzo na Urusi na endapo inaweza kuchangia katika kuyafanya mazungumzo yanayoendelea huko Abu Dhabi kuwa bora zaidi, basi itafanya hivyo.

Merz lakini amesema kwamba hawatoanzisha mazungumzo sambamba na hayo yanayoendelea huko Umoja wa Falme za Kiarabu katika juhudi za kuvimaliza vita vya Urusi nchini Ukraine.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz (katikati) akikamilisha ziara yake ya Ghuba huko Abu Dhabi
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz (katikati) akikamilisha ziara yake ya Ghuba huko Abu DhabiPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Ukraine inajaribu kutatiza mchakato wa amani

Kauli hii ya Merz inakuja wakati ambapo Urusi kupitia msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, imeyataja mazungumzo hayo ya Abu Dhabi yanayojumuisha maafisa wa Urusi, Ukraine na Marekani kuwa yenye tija mno.

Peskov ameyasema haya huku waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov akiituhumu Ukraine kwa kuhusika katika kile alichokiita “tukio la kigaidi” la kujaribu kumuua jenerali wa intelijensia wa Urusi, Vladimir Alekseyev.

“Ila tukio hili la kigaidi kwa mara nyengine linathibitisha dhamira ya utawala wa Zelenskiy ya uchokozi wa mara kwa mara ili kutatiza mchakato wa majadiliano unaoendelea, na nia yake ya kufanya chochote kile ili uwashawishi wafadhili wake wa Magharibi, pamoja na Marekani ilimradi tu mwafaka usipatikane,” alisema Lavrov.

Maafisa wa uchunguzi nchini Urusi wanasema Alekseyev, ambaye ni naibu mkuu wa shirika la ujasusi la kijeshi mjini Moscow, GRU, amepigwa risasi na mtu asiyejulikana Ijumaa katika jumba moja la makaazi mjini Moscow.

Maafisa hao wanasema mshukiwa wa tukio hilo alitoweka na jenerali huyo sasa amelazwa hospitalini, huku uchunguzi ukiendelea na Rais Vladimir Putin akiendelea kuarifiwa.

Ukraine bado haijatoa tamko lolote kuhusiana na tukio hilo. Ukraine lakini imekiri kuhusika mara kadhaa na mauaji ya maafisa kadhaa wa kijeshi nchini Urusi tangu nchi hiyo ilipoivamia mnamo Februari 2022.

Mashambulizi na mauaji yaendelea uwanja wa mapambano

Hayo yakiarifiwa, watu kadhaa wameuwawa nchini Ukraine kufuatia mashambulizi ya Urusi katika eneo la Zaporizhzhya. Kulingana na gavana wa eneo hilo Ivan Fedorov, wapenzi wawili walishambuliwa kwa droni ya Urusi katika mji wa Vilniansk.

Katika shambulio jengine katika eneo hilo hilo, mvulana mwenye umri wa miaka 14 amejeruhiwa na huduma za umeme kukatwa katika karibu nyumba 12,000 za makaazi kufuatai mashambulizi ya Urusi.

Wakaazi wa jumba moja huko Kyiv wakitazama uharibifu uliotokana na shambulizi la Urusi
Wakaazi wa jumba moja huko Kyiv wakitazama uharibifu uliotokana na shambulizi la UrusiPicha: Gleb Garanich/REUTERS

Nako Dnipropetrovsk shirika la ulinzi wa raia la Ukraine linasema mtu mmoja ameuwawa na wengine 4 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya makombora ya Urusi.

Na nchini Urusi gavana wa eneo la Belgorod Vyacheslav Gladkov ameripoti uharibifu mkubwa uliofanywa katika miundo msingi ya nishati katika mji mkuu wa eneo hilo na wilaya kadhaa.

Gladkov amesema huduma za umeme bado zilikuwa hazijarudi kufikia asubuhi ya Ijumaa.

Gavana wa eneo la Bryansk naye amesema nyumba kadhaa zimeachwa bila umeme kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Ukraine.

Vyanzo: DPA/Reuters/AFP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *