Je, nini maana ya vita vya kieneo na ni vya aina gani?

Kwa kuzingatia mivutano na vitisho vya mara kwa mara vya Marekani dhidi ya Iran, Tehran imeonya kuwa hujuma yoyote ya kijeshi ya Marekani dhidi yake itachochea vita vya kieneo. Sasa swali ni je, vita vya kikanda ni nini na vinapiganwaje?

Vita vya kieneo ni aina ya mapigano ya silaha ambayo, badala ya kuzihusisha nchi mbili zinazopigana, hupanuka kijiografia na kulihusisha eneo zima, kuzikumba nchi au wahusika wengi kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, ambapo matokeo yake huathiri eneo kubwa zaidi nje ya mipaka na uwanja mkuu wa vita. Kwa kawaida vita hivi hupiganwa kutokea pande kadhaa kwa wakati mmoja, na huwa haviwezi kudhibitiwa na wahusika wakuu. Ili kufahamu vizuri vita hivi na namna vinavyopiganwa, ni vizuri tuvichambue katika mitazamo minne mikuu.

Upanukaji wa kijiografia na ujumuishaji wa pande nyingi:

Sifa ya kwanza ya vita vya kieneo ni kupanuka na kuvuka kwake mipaka ya kijiografia ya nchi mbili zinazopigana. Kwa mfano, mzozo ulioanza kati ya nchi mbili unaweza kuenea haraka na kulikumba eneo zima kutokana na uwepo wa vituo vya kijeshi vya mmoja wa wahusika, katika ardhi za nchi au serikali za upande wa tatu, au kutokana na mikataba ya kiulinzi na kiusalama kati ya nchi hizo na moja ya madola makubwa ya kigeni. Katika hali hiyo, sio tu kambi za kijeshi, bali nchi au serikali yoyote inayotoa ardhi, anga au rasilimali zake kwa nchi chokozi inaweza kuchukuliwa kuwa sehemu ya uwanja wa vita. Hali hii huunda ngome kadhaa za vita na hivyo kuondoa uwezekano wa kudhibitiwa au kupunguzwa eneo la mzozo.

Idadi na anuwai ya wachezaji:

Wahusika katika vita vya kikanda sio tu vikosi rasmi vya serikali. Mitandao ya kikanda, vikundi vya mapambano na muqawama, vikosi vya niaba na miungano ya kimataifa inaweza kushiriki kikamilifu katika migogoro hiyo. Hili huondoa vita kutoka mkondo wake wa kawaida na kuvigeuza kuwa mzozo tata, usio na mlingano na ulioenea sehemu kubwa. Kuhusiana na hili, huenda nchi isishiriki katika mapigano ya moja kwa moja peke yake, bali mitandao ya washirika au makundi yanayoiunga mkono katika eneo yanaweza kuhusika, na kuisaidia nchi hiyo katika vita vya pande nyingi.

Manowari ya Marekani, chanzo kikuu cha chokochoko zake katika eneo

Atambulisho wa kutowiana mzozo:

Si lazima vita vya kikanda viwe na mlingano. Upande mmoja unaweza kutaka kufikia ushindi wa haraka vitani kwa kutegemea ubora wa kiteknolojia, nguvu za anga na majini, wakati upande mwingine unaweza kugeukia vita visivyo vya mlingano kwa kutegemea kina cha kimkakati, eneo lake la kijiografia, uwezo wa makombora, ndege zisizo na rubani na silaha kama vile vita vya mtandaoni na kuvuruga usalama wa njia muhimu za usafiriji nishati, yakiwemo malango-bahari ya kimataifa. Katika hali kama hiyo, vita vinaweza kufafanuliwa kama “vita vya jiografia dhidi ya teknolojia” au uvurugaji wa miundombinu muhimu ya kiuchumi na nishati, na hivyo kuutatizo upande ulio na teknolojia ya hali ya juu zaidi.

Matokeo yanayovuka mipaka na yasiyo ya kijeshi:

Kipengele muhimu zaidi cha vita vya kikanda ni upeo mkubwa wa matokeo yake. Madhara ya vita hivyo si ya kijeshi tu, bali taathira zake za kiusalama, kiuchumi na kisiasa huvuka haraka mipaka ya eneo la vita. Kutokuwa salama njia muhimu za usafirishaji wa nishati na biashara ya kimataifa kunaweza kutatiza usambazaji wa rasilimali na kuongeza bei kwa haraka, jambo ambalo bila shaka linaweza kutoa mashinikizo makubwa kwa uchumi wa dunia. Kwa mfano, kukosekana usalama katika njia muhimu kama Lango-Bahari la Hormuz, ambapo karibu asilimia 20 ya nishati duniani hupitia, kutakuwa na athari ya moja kwa moja na ya haraka kwa uchumi wa nchi zote zinazotegemea nishati ya mafuta. Pia, vita hivi vinaweza kuchochea tofauti za kikabila, kidini na kiitikadi katika eneo na hivyo kuvuruga amani na utulivu kwa miongo kadhaa.

Tahadhari ya vita vya kikanda

Ni wazi kwamba vita vya kikanda sio vita vikubwa tu, bali huandamana na mabadiliko ya ubora katika mfumo wa vita vyenyewe. Hii ni kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kwamba wigo wa vita hivi huenda ukatoka nje ya udhibiti wa wahusika, wahusika wasio wa kiserikali na wa kikanda wakapata nafasi zaidi katika maamuzi, mbinu za vita visivyo vya uwiano zikatawala na matokeo yake yakaziathiri nchi zote za kanda na hata jamii ya kimataifa. Sifa hizi kuhusu vita vya kikanda zinaonyesha wazi ni kwa nini onyo kuhusu kugeuzwa mzozo wa sasa kuwa vita vya kikanda kwa hakika ni onyo la kimkakati kuhusu uwezekano wa kutodhibitiwa matokeo yake na si tishio la kijeshi tu.

Kwa kutilia maanani kushadidi vitisho vya kijeshi vya Washington dhidi ya Tehran na kutumwa vikosi na zana za kijeshi katika eneo la Asia Magharibi, viongozi wakuu wa Iran wameonya dhidi ya kugeuzwa uvamizi wowote wa Marekani dhidi yake kuwa vita vya kieneo. Kuhusiana na suala hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba aliyotoa tarehe 1 Februari mwaka huu aliashiria juhudi za Marekani za kutaka kuimeza Iran na mapambano ya taifa la Iran dhidi ya ulafi na tamaa hiyo kuwa sababu kuu ya makabiliano ya miaka 47 kati ya Iran na Marekani. Ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya Wamarekani na kusema: “Wamekuwa wanaposema kwamba “machaguo yote yako mezani” ili kulitia hofu taifa la Iran, wajue kwamba wakianzisha vita mara hii, vitakuwa “vita vya kieneo”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *