
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema, nguvu ya serikali ipo kuzilinda demokrasia na “mashambulizi zinayopata” na kuwalinda watoto na vijana na “ulimwengu wenye madhara makubwa, usioadhibiwa” ambavyo ndivyo imekuwa mitandao ya kijamii hivi sasa.
Akihutubia kikao cha ufungaji wa Kongamano la 8 la Kitaifa la Viwanda mjini Bilbao jana Alkhamisi, Sanchez ametetea mipango ya serikali ya kuyawekea kanuni kali zaidi majukwaa ya kidijitali, hasahasa kwa ajili ya kuwalinda watoto.
Gazeti la La Voz de Asturias linalochapishwa nchini Uhispania limemnukuu Sanchez akisema: “nguvu ya serikali ipo kuzilinda demokrasia na mashambulizi zinayopata, na pia watoto na vijana na ulimwengu huo wenye sumu, usioadhibiwa, ambavyo kwa masikitiko ndivyo mitandao ya kijamii imekuwa”.
Waziri Mkuu wa Uhispania ametoa matamshi hayo huku ukishuhudiwa mgongano kati ya umma na shakhsia mashuhuri wa teknolojia kuhusu pendekezo la serikali ya nchi hiyo la kuweka mipaka ya utumiaji wa mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16.
Sanchez ametoa jibu kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa ukosoaji wa mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Telegram Pavel Durov, ambaye siku ya Jumatano aliwaonya watumiaji wa mitandao kwamba kanuni zilizopangwa kuwekwa na Uhispania zinatishia “uhuru wa intaneti” na kusababisha hatari ya kuigeuza nchi hiyo kuwa “serikali ya upelelezi.”
Waziri Mkuu huyo wa Uhispania ameandamwa pia na mashambulizi ya mmiliki wa mtandao wa X na bilionea wa teknolojia Elon Musk, ambaye mapema wiki hii alimwita Sanchez “fashisti mkiritimba” na “mtawala wa kiimla.”
Sanchez amekanusha madai kwamba udhibiti unaowekwa ni sawa na uchujaji au ukiritimba na kutanabahisha kwamba mjadala unapaswa ujikite katika kuzingatia madhumuni ya uvumbuzi wa teknolojia.
“Wengine wanasema kanuni ni udhibiti, kwamba kufanya siasa ni ukiritimba, kwamba kuweka taratibu kunabana uvumbuzi. Lakini masuali makuu mara nyingi huwa hayaulizwi kamwe. Tunautaka uvumbuzi huu kwa ajili ya nini? Kupanua haki au kuweka haki hizo hatarini? Kuimarisha demokrasia au kuiharibu? Kuboresha maisha ya watu au kwa ajili ya wachache kujaza mifuko yao?” amehoji waziri mkuu huyo wa Uhispania.
Sanchez amekosoa kile alichokielezea kama nguvu isiyodhibitiwa ya wasomi wa teknolojia, akiwashutumu kwa kueneza taarifa potofu na kutumia vibaya taarifa binafsi za watu.
Amesisitiza kwa kusema: “Hawatatuvunja nguvu, kwa sababu sauti ya mantiki, ya walio wengi kijamii na ya demokrasia, haitanyamazishwa na kundi la wachache la teknolojia ya algoriti”…/