Serikali ya Cuba imetangaza kifurushi cha hatua za dharura siku ya Ijumaa katika nyanja za elimu, ajira, na usafiri ili kushughulikia mgogoro wa nishati ambao nchi inapitia chini ya shinikizo kutoka Marekani.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Shinikizo hizi “zinatulazimisha kutekeleza mfululizo wa maamuzi, kwanza kabisa ili kuhakikisha uhai wa nchi yetu na huduma za msingi, bila kusahau maendeleo,” Naibu Waziri Mkuu Oscar Pérez-Oliva Fraga ameiambia televisheni ya serikali.

Miongoni mwa hatua zilizotangazwa ni pamoja na kupunguzwa kwa wiki ya kazi katika makampuni yanayomilikiwa na serikali hadi siku nne, kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi, vikwazo vya mauzo ya mafuta, kupunguzwa kwa huduma za mabasi na treni kati ya mikoa, na kufungwa kwa baadhi ya vituo vya watalii. Katika elimu, siku za shule zitakuwa fupi, na vyuo vikuu vitafanya kazi katika muundo mseto (ujifunzaji mseto). Hatua hizi zinalenga kuokoa mafuta ili kukuza “uzalishaji wa chakula na umeme” na “kulinda shughuli muhimu zinazozalisha fedha za kigeni,” ameelezea Bw. Pérez-Oliva Fraga.

Ushuru wa Marekani

Ingawa kisiwa hicho chenye wakazi milioni 9.6, chini ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani tangu mwaka 1962, kimekuwa kikikumbwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi kwa miaka sita iliyopita, Washington imeongeza shinikizo kwa serikali ya kikomunisti huko Havana katika wiki za hivi karibuni.

Baada ya kusitisha usafirishaji wa mafuta kutoka Venezuela kufuatia kukamatwa kwa rais Nicolas Maduro mapema mwezi Januari, Donald Trump wiki iliyopita alisaini agizo la utendaji linaloonyesha kwamba Marekani inaweza kuweka ushuru kwa nchi zinazouza mafuta kwa Havana. Pia alidai kwamba Mexico, ambayo imekuwa ikiipa Cuba mafuta tangu mwaka 2023, ingeacha kufanya hivyo.

Ili kuhalalisha sera yake, Washington inataja “tishio la kipekee” linalotokana na Cuba, kisiwa cha Karibiani kilichopo kilomita 150 tu kutoka pwani ya Florida, kwa usalama wa taifa wa Marekani. Kwa upande wake, Havana inamtuhumu Donald Trump kwa kutaka “kuzima” uchumi wa kisiwa hicho, ambapo kukatika kwa umeme na uhaba wa mafuta, ambao tayari umejirudia katika miaka ya hivi karibuni, kumekithiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *