
Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuwa limehusika na shambulio lililolenga msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Khadijatul Kubra mjini Islamabad huko Pakistan na kuua makumi ya watu wakati wa Swala ya Ijumaa.
Ijumaa ya jana, polisi na maafisa wa serikali ya Pakistan walitangaza kuwa shambulio la kujilipua kwa bomu liliua watu wasiopungua 31 na kujeruhi karibu wengine 170 wakati wa Swala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Bibi Khadija (as).
Vyanzo vya usalama vya Pakistan vimeripoti kwamba “mshambuliaji alijilipua kwa mabomu kwenye lango la msikiti huo uliopo katika eneo la Tarlai nje kidogo ya Islamabad, wakati aliposimamishwa na walinzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Asif ameandika kwenye jukwaa la X kwamba mshambuliaji huyo alijilipua katika safu ya mwisho ya waumini waliokuwa wakitekelezwa Swala ya Ijumaa.
Amesema kwamba gaidi huyo alikuwa na historia ya kusafiri nchini Afghanistan, na ameilaumu nchi jirani ya India kwa kufadhili shambulio hilo, bila kutoa ushahidi.
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya India imelaani shambulio hilo na kupuuza taarifa ya Pakistan, akiitaja kuwa “isiyo na msingi”.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha miili ya watu iliyojaa damu ikiwa imelala sakafuni msikitini, ikiwa imezungukwa na vioo vilivyovunjika.
Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan amesema “kuwalenga raia wasio na hatia ni uhalifu dhidi ya ubinadamu”.