
Mapigano, mashambulizi na uporaji wa vituo vya kibinadamu na vya afya pamoja na vikwazo vya usafiri na hali ya kutokuwepo kwa usalama katika njia muhimu za usambazaji vinaathiri kwa kiasi kikubwa operesheni za kibinadamu na kusababisha kusitishwa kwa huduma muhimu, hali inayowaweka raia, wakiwemo wafanyakazi wa misaada, katika hatari kubwa.
Tangu mwishoni mwa Desemba, takribani vituo 11 vya huduma za afya vimeshambuliwa katika Jimbo la Jonglei, jambo lililosababisha kuvurugika kwa huduma za kuokoa maisha. Mashambulizi hayo pia yamehusisha kutekwa kwa magari 12, likiwemo gari la wagonjwa. Katika wiki moja iliyopita pekee, matukio kote nchini yamejumuisha mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya msafara wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), shambulio la anga dhidi ya hospitali inayoendeshwa na shirika la Madaktari waio na mikapa, Médecins Sans Frontières, pamoja na kuchomwa kwa ofisi ya shirika la watoto la Save the Children na kuharibiwa kwa kituo chake cha afya.
Kupuuza huku waziwazi shughuli za matibabu na misaada ya kibinadamu hakukubaliki na lazima kukome mara moja. Kazi hizi zinapaswa kuwezeshwa na kuheshimiwa.
Zaidi ya watu 370,000 wameripotiwa kuyahama makazi yao kutokana na mapigano kote nchini mwaka huu pekee, wakiwemo zaidi ya watu 280,000 katika Jimbo la Jonglei, wakati mlipuko wa kipindupindu ukiendelea kuongezeka kwa kasi.
“Katibu Mkuu anazitaka pande zote kusitisha mara moja na kwa dhati operesheni zote za kijeshi, kupunguza mvutano kupitia mazungumzo, kuheshimu sheria za kimataifa, kuwalinda raia, na kuhakikisha upatikanaji salama na endelevu wa misaada ya kibinadamu pamoja na usalama wa wafanyakazi wa misaada na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na mali zao.” Imesisitiza taarifa hiyo.