Dar es Salaam. Akiwa anaelekea kutimiza miaka 10 tangu amepata umaarufu kupitia muziki, Nandy amejipambanua kati ya wasanii wachache wa Bongofleva wasioona aibu kusema wameandikiwa wimbo na mtu fulani.

Na ndivyo alivyofanya katika wimbo wake mpya, Asante (2026), ukiwa ni mwendelezo wa kutoa nafasi kwa wasanii na waandishi wengine wa nyimbo kumletea mawazo mapya katika muziki wake.

Kwa mujibu wa Nandy, wimbo huu mpya ‘Asante’ ameandikiwa na Obby Alpha ambaye ni mwimbaji wa muziki wa Injili aliyetamba na wimbo wake, Bora Kushukuru (2023).  

Asante ni wimbo unaogusa moyo ukiwa na ujumbe wa faraja uliojikita katika imani na shukrani, ukisisitiza kuwa kila hatua iliyopigwa kivyovyote vile iliongozwa na neema ya Mungu.

Katika wimbo huu wa kuhamasisha, Nandy anamshukuru Mungu kwa uhai, ulinzi na safari yote aliyopitia iwe ni wakati wa changamoto au wa ushindi.
Kupitia mdundo mzuri na sauti yenye kugusa hisia, unaakisi nyakati ngumu maishani zilizogeuka kuwa mafunzo.

Chini ya utayarishaji wake Kimambo, wimbo huu unatoa ujumbe mzito wa kuthamini, ukiwakumbusha wasikilizaji kusimama na kumshukuru Mungu bila kujali hali wanazopitia.

Wimbo huu unahamasisha tumaini, unyenyekevu na imani katika mpango wa Mungu, ukiwahimiza watu wote kutambua baraka zao na kubaki na shukrani katika nyakati zote za maisha.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Nandy kuja na muziki wa namna hii, alishatoa hadi Extended Playlist (EP), Wanibariki (2021) ikiwa na nyimbo tano.

Mradi huo ulikuja miaka mitatu baada ya kuurudia (cover) wimbo wa Angel Benard, Nikumbushe Wema Wako (2016), kisha akashinda Maranatha Awards 2018 katika kipengele cha Best Worship Song Cover.

Ila ikumbukwe Obby si msanii wa kwanza wa Injili kumwandikia wimbo mwimbaji wa Bongofleva kwani kipindi Goodluck Gozbert akisimama kama mtayarishaji akitambulika kwa jina la Lollipop, alifanya hivyo pia.

Baadhi ya nyimbo za Bongofleva alizoandika Goodluck Gozbert na zikafanya vizuri ni Moyo Mashine (2016) wake Ben Pol, na Basi Nenda (2014) wa Mo Music na ndio ulimtoa kimuziki msanii huyo.

Kwa ujumla Obby anaungana na mastaa kama Billnass, Marioo, Kusah, Lody Music na Jay Melody ambao wamewahi kumwandikia Nandy nyimbo kwa nyakati tofauti.

Rapa Billnass ndiye alimwandikia Nandy wimbo wake, Dah! (2024) ukiwa ni wimbo wa tatu kumwandikia mpenzi wake huyo ambaye walifunga ndoa Julai 2022 baada ya takribani miaka saba ya uhusiano.

Nyimbo nyingine ambazo Billnass kamwandikia Nandy ni Bugana (2019) walioshirikiana, pia kuna New Couple (2021) kutoka katika EP yake ya pili, Taste (2021).

Hadi sasa Jay Melody ndiye msanii aliyemwandikia Nandy nyimbo nyingi na zote zikafanya vizuri. Jay kamwandikia nyimbo nne; Kivuruge (2017), Njiwa (2018), Hallelujah (2019) na Do Me (2020).

Marioo amemwandikia Nandy wimbo wake, Wasikundanganye (2017), ila huu wimbo tayari Marioo alikuwa ameshaurekodi ila Nandy alipousikia ukaupenda na kuomba aurudie uwe wake.  

Naye Lody Music amemwaandikia Nandy wimbo, Napona (2022) akimshirikisha Oxlade kutokea Nigeria, na huu ndio wimbo uliofanya vizuri zaidi katika EP yake ya tatu, Maturity (2022).

Kwa upande Kusah, ndiye ameandika wimbo wa Nandy, Nibakishie (2020) akimshirikisha Alikiba ikiwa ni kolabo yao ya kwanza kabla ya kufuatia nyingine mbili.  

Ikumbukwe Kusah amewaandikia wasanii wengine, mwingine ni Ruby aliyeandikiwa wimbo wake maarufu, Ntade (2018) ambao ulifanya vizuri sana na kumrudisha katika muziki baada ya ukimya mrefu.

Wakati baadhi ya wasanii wenye majina makubwa kila mara akikataa kuweka wazi kuwa wameandikiwa nyimbo hadi kuleleta migogoro na waandishi wa nyimbo hizo, kwa Nandy mambo ni tofauti kabisa.

Nandy alipata umaarufu kimuziki kupitia wimbo wake, Nagusagusa (2016) uliotayarishwa na Emma The Boy chini ya Tanzania House of Talent (THT), huku video yake ikiongozwa na Director Hanscana.

Video hiyo ilitoka Julai 22, 2016 ikiwa ni takribani miezi minne tangu Nandy kushika nafasi ya pili shindano la kwanza la karaoke Afrika, na kupewa nafasi ya kupata mafunzo chini ya lebo ya Chocolate City.

Kufanya vizuri kwa huo, kulipelekea kuchaguliwa kuwakilisha nchi katika mradi wa Coke Studio Africa 2017, ambako alifanya show ya kuvutia sana akishirikiana na mwimbaji kutokea Ethiopia, Betty G.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *