Katika taarifa yake iliyotolewa tarhe 6 Februari jijini Amman, Jordan, Mkurugenzi wa Kanda wa UNICEF kwa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Edouard Beigbeder, amesema watoto katika eneo hilo wanaendelea kuuawa, kujeruhiwa, kulazimika kuhama makazi yao, kukamatwa na kuzuiliwa, pamoja na kunyimwa huduma muhimu kama vile afya na elimu, huku migogoro ikizidi au kuendelea katika nchi kadhaa.

Syria

Nchini Syria, mapigano mapya kaskazini-mashariki mwa nchi yamesababisha karibu watu 200,000 kuyahama makazi yao, takribani nusu yao wakiwa ni watoto, na kuvuruga huduma muhimu. UNICEF imeripoti kuwa angalau watoto watano wamefariki dunia katika Ain Al Arab/Kobani kutokana na ukosefu wa huduma za afya na mahitaji ya majira ya baridi.

Sudan

Nchini Sudan, hali imeendelea kuwa mbaya kwa watoto. Mwezi Januari 2026 pekee, takribani watoto 20 waliuawa, wengi wao katika majimbo ya Kordofan na Darfur. Mamilioni ya watoto wanahitaji msaada wa kuokoa maisha, huku njaa ikithibitishwa katika Al Fasher, Darfur Kaskazini, na Kadugli, Kordofan. Takribani maeneo 20 mengine yako katika hatari ya kukumbwa na njaa kutokana na migogoro inayozuia usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

Iran

Nchini Iran, matukio ya hivi karibuni yamekuwa na athari kubwa kwa watoto na vijana. Zaidi ya watoto 144 wameripotiwa kuuawa, huku wengine wengi wakiripotiwa kujeruhiwa au kuzuiliwa. UNICEF imesema inaendelea kuishinikiza serikali ya Iran kulinda watoto dhidi ya vurugu, ikiwemo kusitisha kukamatwa na kuzuiliwa kwa watoto, na imetoa wito wa kupunguzwa kwa mvutano ili kuepusha madhara zaidi.

Gaza

Katika Ukanda wa Gaza, licha ya kuwepo kwa usitishaji mapigano dhaifu uliosababisha maboresho madogo, hali bado ni tete na hatari kwa watoto wengi. Tangu mwanzo wa mwaka huu, watoto 37 wameripotiwa kuuawa, huku mashambulizi ya anga yakiendelea na mifumo ya afya, maji na elimu ikiwa imeharibiwa vibaya. UNICEF imesisitiza kuwa usitishaji mapigano lazima udumu ili kukomesha mateso ya watoto wa Gaza.

Ukingo wa Magharibi

Katika Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Jerusalem Mashariki, ongezeko la vurugu limeendelea kudhoofisha usalama wa watoto na kuacha familia katika hofu na wasiwasi wa kudumu. Mnamo Januari, watoto wawili waliuawa na wengine 25 kujeruhiwa.

Katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, migogoro ya muda mrefu na mazingira dhaifu inaendelea kuongeza mahitaji ya kibinadamu. Nchini Yemen, watoto wanaendelea kukabiliwa na migogoro mingi ikiwemo vita vinavyoendelea, matatizo ya kiuchumi na utapiamlo ulioenea. Nchini Lebanon, familia bado zinajitahidi kupona kutokana na vita vya hivi karibuni huku zikiishi kwa hofu ya mashambulizi mapya.

UNICEF imelaani vikali aina zote za vurugu dhidi ya watoto, ikiwemo mauaji na ulemavu wa kudumu, ikizitaja kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto usiokubalika kamwe. Shirika hilo limezitaka serikali na pande zote zinazohusika katika migogoro kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, na kuchukua hatua za haraka kukomesha mauaji, majeraha, kukamatwa, kuzuiliwa na kuwatia watoto hofu na majeraha ya kisaikolojia.

“Watoto wote wanachohitaji zaidi ni amani,” anasema Beigbeder.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *