Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Binadamu ya Al-Dameer amekosoa vikali utaratibu wa sasa wa kivuko cha Rafah, akikiita “tasa na hatari” na kuonya kwamba utaratibu wa sasa umesababisha ongezeko lisilotarajiwa la idadi ya vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani katika Ukanda wa Gaza.

Alaa Al-Skafi, mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Dameer, ametangaza kwamba zaidi ya wagonjwa 11,000 wa saratani katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na hatari kubwa ya kifo. Amesisitiza kwamba akiba ya asilimia 70 ya dawa muhimu za saratani sasa imefikia “sifuri,” na eneo hilo halina vifaa vya kugundua mapema na mashine za MRI.

Kulingana na ripoti hii, Al-Skafi ameutaja uharibifu wa vituo maalum vya matibabu ya saratani, ikiwa ni pamoja na “Hospitali ya Urafiki kati ya Uturuki na Palestina” na wodi za saratani katika hospitali za “Ulaya Gaza” na “Al-Rantisi”, kama sehemu ya sera ya mauaji ya kimbari inayolengwa na jeshi la Israeli.

Amesema kwamba kuwazuia wagonjwa kuondoka kwa matibabu ni “mauaji ya moja kwa moja” na mfano dhahiri wa uhalifu wa kivita na ukiukaji wa Mkataba wa Nne wa Geneva.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Dameer, ameashiria takwimu rasmi na kutangaza kwamba zaidi ya wagonjwa 3,000 wamekuwa wakisubiri ruhusa ya kuondoka na kupelekwa nje ya nchi kwa miaka miwili sasa, lakini kutokana na kuchelewa na kuzingirwa kikatili, hakuna uwezekano wa kuwaokoa.

Afisa huyo wa haki za binadamu ametoa wito kwa Shirika la Afya Duniani, Baraza la Usalama, na mashirika ya kimataifa kuweka shinikizo kwa utawala wa Kizayuni ili kuandaa njia ya kupeleka wagonjwa mara moja kupitia kivuko cha Rafah, na kuchukua hatua za haraka kujenga upya mfumo wa afya unaoporomoka wa Gaza na kutoa dawa muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *