Barcelona,Hispania. Barcelona imetangaza kujiondoa rasmi kwenye mradi wa Ligi Kuu ya Ulaya (Super League), hatua inayoiwacha Real Madrid kuwa klabu pekee iliyosalia katika mpango huo.

Jumla ya klabu 12 zilitangaza kujiunga na mashindano hayo mwaka 2021 ikiwa pamoja na Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham na klabu nyinginine kubwa barani Ulaya lakini nyingi zilijiondoa baada ya mashabiki wao kupinga vikali mpango huo.

Atletico Madrid, AC Milan na Inter Milan nazo zilikuwemo lakini zilijiondoa na kuziacha Barcelona, Real Madrid na Juventus. Hata hivyo, baadae vigogo hao wa Italia walijiondoa mwaka 2024.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi asubuhi, Barcelona ilithibitisha kujiondoa kwao kwenye mradi huo, hatua inayomwacha Real Madrid kama pekee iliyosalia.

“FC Barcelona inatangaza rasmi kwamba leo imewaarifu Kampuni ya European Super League pamoja na klabu husika kuhusu kujiondoa kwake kwenye michuano ya European Super League.”

Rais wa Barcelona, Joan Laporta, mwaka 2023 alisema kuwa bado anaamini Super League itazinduliwa na itafanyika tu.

Hata hivyo, mwaka jana Laporta alisisitiza kuwa Barcelona ilikuwa inataka kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA jambo lililoashiria nia yao ya kujiondoa katika Super League.

Kujiondoa kwa Barcelona kwenye Super League kunakuja siku nne baada ya Laporta kuthibitisha kujiuzulu kwa bodi yake ya uongozi, jambo linalolenga kumpa nafasi ya kugombea tena urais wa klabu hiyo katika uchaguzi wa mwezi ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *